Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons yashikilia faili la ajira ya Malale JKT

Prisons Kosa.jpeg Prisons yashikilia faili la ajira ya Malale JKT

Wed, 13 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Leo huenda ikawa siku ya mwisho ya kocha Malale Hamsini kuifundisha JKT Tanzania kwa msimu huu atakapoiongoza katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuanzia saa 10:00 jioni.

Mwanaspoti linajua JKT Tanzania inapanga kumfuta kazi Malale kama atapoteza mechi ya leo, kutokana na muendelezo wa matokeo mabaya ya kikosi hicho alichokifundisha tangu msimu uliopita kikiwa Championship na kukipandisha Ligi Kuu.

Malale msimu huu ameiongoza JKT kwenye mechi 19 za ligi na kushinda nne, sare saba na kupoteza nane jambo ambalo uongozi wa timu hiyo hauridhiki nalo kwani wakati msimu unaanza ilimtimizia matakwa yake yote kocha huyo.

"Maji yanazidi unga. Tulimpa kila kitu alichokitaka, kuanzia wachezaji hadi kambi lakini leo mambo yanazidi kuwa magumu. Nadhani mechi ya leo ndiyo itaamua hatma yake ndani ya kikosi chetu, tuko tayari kuachana naye kama tutafungwa," alisema mmoja wa vigogo wa timu hiyo ya jeshi ambayo jana imekabidhiwa basi jipya na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Generali Jacob John Mkunda.

Kabla ya mechi ya leo, JKT imecheza mechi 10 mfululizo za ligi bila ushindi ikiambulia sare tano na kupokea vichapo vitano.

Timu hiyo ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa ya pili kutoka mkiani juu ya Mtibwa Sugar tu inayofyata mkia na alama 15 huku JKT ikiwa nazo 19.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live