Baada ya kuonja ushindi wa kwanza Ligi Kuu msimu huu, Tanzania Prisons imesema kwa sasa inasaka mwarobaini wa kupunguza kufungwa na kuongeza idadi kubwa ya mabao.
Timu hiyo haikuwa na mwanzo mzuri baada ya kucheza mechi nne mfululizo bila kupata ushindi ikitoa sare moja na kupoteza mitatu kabla ya juzi kuonja ladha ya pointi tatu ilipoichapa Mtibwa Sugar 3-2.
Pamoja na ushindi huo ambao uliitoa mkiani na kuipandisha nafasi ya 13 kwa pointi nne, lakini timu hiyo bado ndio kinara wa kuruhusu idadi kubwa ya mabao (11), ikifuatiwa na Mtibwa Sugar iliyofungwa 10 katika mechi tano zilizochezwa hadi sasa.
Nahodha na beki wa timu hiyo, Jumanne Elfadhil amesema baada ya ushindi wao wa kwanza sasa wanaanza kusaka heshima nyingine ya kupambana kutoruhusu mabao mengi.
"Tumeruhusu mabao mengi jambo ambalo si afya sana kwetu, lazima tukae kujiuliza na kurekebisha makosa ili kuanzia mechi ijayo dhidi ya JKT Tanzania Oktoba 24, tushinde kwa idadi kubwa ya mabao ila tusifungwe," amesema beki huyo msitaarabu.
Kwa upande wake kocha mkuu wa timu hiyo, Fred Felix 'Minziro' amesema wakati wakisaka mwarobaini wa kutofungwa idadi kubwa ya mabao, lakini wanahitaji kuendeleza ushindi unaoambatana na mabao mengi.
"Wakati tukipambana kutoruhusu idadi kubwa ya mabao, lakini lazima tutafute idadi kubwa ya mabao, benchi la ufundi linaendelea kusuka timu kuhakikisha tunafikia malengo," amesema Minziro.