Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons yaipania Simba

Tz Prisons Mil30 Prisons yaipania Simba

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Prisons itapambana na Simba leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa huku kocha wa maafande hao, Patrick Odhiambo akisema kuwa ana kazi ngumu kufuta rekodi mbaya kila wanapokutana na wapinzani wao jijini Dar es Salaam kwa miaka 20 sasa.

Prisons licha ya mara nyingi kuifunga Simba kwenye uwanja wao wa Sokoine, Mbeya lakini inakutana na mfupa mgumu inapocheza na timu hiyo Dar es Salaam.

Mara ya mwisho Prisons kuifunga Simba Dar es Salaam ni Agosti 8, 2002, ikiwa chini ya kocha Fred Felix Minziro na kushinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Herry Morris na Primius Kasonso.

Baada ya hapo kwa miaka 20 sasa, Prisons imekuwa ikikumbana na vipigo au sare kila inapocheza na Simba jijini Dar es Salaam iwe Uwanja wa Uhuru au wa Mkapa.

Kwa misimu mitano ya karibuni timu hizo zilipokutana Dar es Salaam, Prisons imekubali kipigo katika michezo mitatu huku ikitoka sare michezo miwili.

Msimu wa 2017/2018, ilichapwa mabao 3-0 na Simba, msimu uliofuata wa 2018/2019 ikakubali kipigo cha bao 1-0, msimu wa 2019/2020 timu hizo zilitoka suluhu.

Msimu wa 2020/2021, zilifungana bao 1-1 wakati msimu uliopita Prisons ililala kwa bao 1-0 na sasa inasubiriwa kuona kesho kama itaweza kufuta uteja kwa Simba.

Herry Morris, ambaye alifunga bao mara ya mwisho Simba ilipoichapa Prisons kwenye Uwanja wa Uhuru alisema ni wakati wa timu hiyo kufuta gundu la kutopata ushindi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

“Prisons ya sasa imepoteza ladha yake tofauti na kipindi sisi tunacheza kwani tulikuwa hatuogopi timu yoyote iwe ya ndani au nje ya nchi tulikuwa na kikosi bora sana.

“Ili waweze kuifunga Simba tena inabidi kwanza mchezaji mmoja mmoja wa timu hiyo ajue jinsi ya kucheza na mpinzani wake anapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, hapo wataweza kuutafuna huo mfupa.

“Wapambane hakuna kitu kinachoshindikana, naamini hata mechi ya Ijumaa kama wakijituma, wakiimarisha vizuri eneo lao la ulinzi na kucheza kwa nidhamu na wakitumia nafasi watakazopata wanaweza kushinda hiyo mechi,” alisema Morris.

Kocha wa Prisons, Patrick Odhiambo alisema wanajua wanakutana na timu bora na ngumu lakini wamejipanga kuhakikisha wanafuta gundu la Dar.

Chanzo: Mwanaspoti