Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons yaichapa Dodoma Jiji, watamba kazi ndio imeanza

TZ Prisons Winner Prisons imepata ushindi wa kwanza tangu mwezi Oktoba

Wed, 21 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kusota kwa muda mrefu bila ushindi, hatimaye leo Tanzania Prisons imefufuka na kuibutua Dodoma Jiji mabao 2-0 na kupanda nafasi ya 11 kwa pointi 18.

Mara ya mwisho timu hiyo kupata alama tatu ilikuwa Oktoba 15 ilipoiparua Polisi Tanzania tangu hapo hali ilikuwa tete si shwari kwa kuchezea sare na vipigo.

Matokeo hayo yanaendeleza rekodi kwa Wajelajela hao dhidi ya Dodoma Jiji kwani msimu uliopita ikicheza kwenye uwanja wa Sokoine ilishinda 3-2.

Kama haitoshi Dodoma wanaichangia alama sita msimu huu baada ya mechi ya raundi ya kwanza kupoteza nyumbani katika uwanja wa Liti mkoani Singida mabao 2-1.

Hizi ni baadhi ya dondoo za mpambano huo;

Nahodha wa Dodoma Jiji, Mbwana Kibacha anaungana na nyota wengine wa ligi kuu kukosa penalti na kuifanya timu hiyo kuondoka patupu katika mchezo wa leo ambao kwa kiasi kikubwa walizidiwa na wapinzani.

Bao la Zabona Hamisi dakika ya pili linakuwa la kwanza kwake msimu huu, huku akifikisha asisti tatu tangu ajiunge na Wajelajela hao, huku Samson Mbangula akifikisha mabao matatu.

Kabla ya ushindi wa leo, Prisons ilikuwa imecheza mechi sita mfululizo bila kupata alama tatu, huku kwenye uwanja wa Sokoine ikicheza mechi tisa ikishinda miwili, sare mbili na kupoteza mitano.

Kocha Mkuu wa Prisons, Patrick Odhiambo amesema ilikuwa muda mrefu wamepata ushindi, hivyo pointi tatu za leo zimerejesha ari na morali kikosini kujiandaa na mechi zinazofuata.

“Tulikaa na wachezaji tukawaeleza umuhimu wa mchezo wa leo, niwapongeze kwa kazi nzuri waliyofanya na sasa tunaenda tena kujipanga upya na mechi zinazokuja,” amesema Odhiambo.

Kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope amesema walitarajia mechi kuwa ngumu kutokana na matokeo ya wapinzani yalivyokuwa na kwamba walifanya makosa ambayo yaliweza kuwagharimu.

“Walistahili kushinda tulipambana kutumia mbinu tofauti lakini waliweza kutuzidi hadi mwisho tunakosa penalti ni sehemu ya mchezo tunaenda kujipanga upya,” amesema Liogope

Chanzo: www.tanzaniaweb.live