Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons yahamia kwa Azam

Prisons Vs Azam Prisons yahamia kwa Azam

Thu, 29 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Tanzania Prisons imekiri kuwa inapokutana na Azam huwa inachezea vichapo sasa kesho Ijumaa, inaenda kufuta uteja kwa kupata ushindi licha ya kuwakosa nyota wake saba wenye sababu mbalimbali.

Prisons haijapata ushindi kwa Azam kwa misimu mitatu mfululizo, ambapo mara ya mwisho kushinda ilikuwa April 2, 2019 kwa bao la Jumanne Elfadhil.

Kesho Septemba 30 timu hizo zitakutana kwenye uwanja wa Sokoine ambapo Azam inajivunia rekodi kwa Wajelajela hao ambao msimu uliopita iliwanyuka jumla ya mabao 5-0 ikianza kuwachakaza 4-0 ugenini kwenye uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa kisha kuwatungua 1-0 kwenye uwanja wa Chamazi Dar es Salaam.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Shaban Mtupa amesema kesho hawakubali kupoteza mechi ya pili mfululizo lakini kutokubali tena kuwa wateja kwa wapinzani hao kwani vipigo vimetosha.

Amesema pamoja na maandalizi na matumaini makubwa waliyonayo kufanya kweli, watawakosa nyota wake saba ambao wana sababu mbalimbali ikiwamo majeruhi, kadi nyekundu na majukumu kwenye timu ya Taifa ya Vijana (U20).

"Nurdin Chona, Salum Kimenya na Mussa Mbisa hawa ni majeruhi, Oscar Paul na Edwin Balua wako timu ya Taifa, Michael Masinda ana kadi nyekundu, lakini waliobaki wako tayari kwa mapambano na tunaamini kesho ni ushindi." amesema Mtupa.

Kocha huyo ameongeza kuwa kwa muda waliokaa mapumziko kwa takribani wiki mbili, wamefanyia kazi mapungufu yote hususani sehemu ya ushambuliaji ambao mechi iliyopita na Simba walishindwa kufanya vizuri na kujikuta wakipoteza mechi hiyo kwa bao 1-0.

Naye Nahodha wa timu hiyo, Benjamin Asukile amesema mchezo huo utakuwa wa kisasi kwani wapinzani hao waliwafanyia kitu mbaya msimu uliopita na kwamba baada ya mechi na Simba, kwa sasa stori kubwa kwao kambini ilikuwa ni Azam.

"Itakuwa mechi ya kisasi, Azam walitufanyia kitu kibaya, tumekuwa tukifungwa sana tunapokutana nao, hivyo kesho tunaenda kulipiza, kukosekana kwa baadhi ya wachezaji haiwezi kutuathiri sisi wengine kwa sababu wachezaji wote wa Prisons wanaweza kuanza kikosi cha kwanza" amesema Asukile.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz