Uongozi wa Tanzania Prisons umesema licha ya kuanza vibaya msimu lakini wanashukuru kumaliza vyema msimu, huku ukiweka wazi kuwa tayari umeanza mazungumzo na nyota wao waliofanya vizuri ili kubaki nao msimu ujao.
Prisons haikuwa na mwanzo mzuri chini ya aliyekuwa kocha wao, Patrick Odhiambo ambaye alifurumushwa katikati ya msimu na kumpa majukumu Abdalah Mohamed ‘Bares’.
Baresi tangu alipotua kikosini humo tangu Februali 1, amekuwa na matokeo mazuri na kuifanya timu hiyo kutoka nafasi ya 13 hadi kumaliza nafasi ya nane kwa pointi 37.
Katibu mkuu wa timu hiyo, Ajabu Kifukwe alisema kutokana na kiwango walichoonesha mastaa wao, tayari wameanza mazungumzo kwa wale wanaomaliza mikataba yao ili kubaki msimu ujao.
Alisema wanafanya hivyo ili kumrahisishia kocha kuendelea alipoishia kuliko kuanza kumtafutia wachezaji wengine ambao ataanza upya kutafuta muunganiko hali ambayo inaweza kuwapa wakati mgumu.
“Kwanza tunashukuru na kuwapongeza benchi la ufundi na wachezaji kwa kujituma na kuipa matokeo mazuri timu hadi kumaliza ligi bila presha, tumeanza mipango na maandalizi ya msimu ujao.”
“Moja ya mipango ni kuzungumza na wachezaji ambao mikataba yao imeisha ili tubaki nao kutegemea na ubora walioonesha kwa msimu mzima, lengo ni kumrahishia kocha kazi asianze upya kutafuta muunganiko,” alisema Kifukwe.
Kwa upande wake Baresi alisema anajivunia mafanikio ya muda mfupi kikosini huku akiwashukuru uongozi na mashabiki kwa sapoti na kwamba msimu ujao prisons itafanya vizuri zaidi.
“Ni kweli lazima kujipongeza haikuwa kazi nyepesi lakini tumeweza kumaliza salama, tunaenda kufanya tathimini kisha kukabidhi ripoti kujua msimu ujao tunaanzia wapi,” alisema kocha huyo.