Hali ya Tanzania Prisons kwenye Ligi Kuu Bara imeendelea kuwa tete baada ya kufikisha mechi sita mfululizo bila kupata ushindi ikiambulia sare moja tu jambo linaloiweka kwenye hatari ya kushuka daraja na sasa imeanza kupiga hesabu za vidole ili kujinasua.
Prisons kwa sasa ipo nafasi ya tatu kutoka mkiani (14), na alama 22 baada ya mechi 24 ikiwa imebakiza mechi sita kumaliza msimu na sasa imepanga kushinda walau mechi tatu zijazo ili kurejesha matumaini ya kubaki kwenye ligi.
Akizungumza kocha mkuu wa Wajelajela hao, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema amekubali kwamba, “ligi ni ngumu na tuko sehemu mbaya zaidi, tumebakiza mechi sita ambazo ni ngumu ila ni muhimu sana kwetu, nimekaa na wachezaji wote na kuwaeleza mahitaji yetu na namna tunatakiwa kufanya ili tusishuke.”
“Tunahitaji walau ushindi kwenye nusu ya mechi zilizobaki na baada ya hapo tunaweza kuwa sehemu salama, na hilo tunahitaji kuanza kulifanyia kazi kwenye mechi ijayo.”
Mechi zilizobaki za Prisons ni dhidi ya Namungo ugenini, Ruvu Shooting nyumbani, Geita Gold ugenini, Kagera Sugar ugenini pamoja na KMC na Yanga zote ikiwa nyumbani.
Timu nyingine ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja zikiwa zimebakiza mechi sita tu ni Ruvu, Polisi Tanzania, KMC, Dodoma Jiji, Coastal Union na Mbeya City.