Baada ya kukosa ushindi katika mechi ya kwanza mbele ya Bacca City, leo Tanzania Prisons imefufuka na kuichakaza Nakonde City mabao 3-0 katika mchezo wa ligi ya Mbeya Pre Season.
Mechi hiyo ambayo ilikuwa ya pili kwa timu hizo, Prisons ilianza kwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Bacca City huku Nakonde City ikishinda mbele ya Mbarali mabao 2-1 na kufanya mchezo huo kuwa wa ushindani.
Ikicheza kwa ubora leo kwenye uwanja wa Kipija wilayani hapa, mabao ya Edwine Balua aliyetupia mawili na Zabona Hamis yalitosha kuipa alama tatu na kuiweka pazuri katika kufuzu hatua inayofuata.
Kocha mkuu wa Prisons, Fredi Felix 'Minziro' amesema bado ni mapema sana kuwatabiria makubwa vijana wake akieleza kuwa kadri siku zinavyokwenda wanabadilika.
Amesema kuhusu ishu ya ubingwa ikitokea ni freshi japo kuwa wanatumia michuano hii kuangalia ubora wa nyota wake na kwamba bado hajafunga usajili na sura mpya zitaendelea kuonekana.
"Kila siku lazima kuwapo maboresho na nimefurahi kiwango kimebadilika kwa sababu mechi ya jana hatukufunga bao, leo tunashinda mabao matatu, tunahitaji mechi nyingi za namna hii kutujenga zaidi" amesema Minziro.
"Kuhusu usajili bado hatujamaliza na siwezi kulielezea zaidi kwakuwa lipo kwenye mchakato, tunafanya mambo kulingana na uhitaji wa timu, kimsingi tunaendelea kujipanga" amesema kocha huyo.