Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons wakubali yaishe, Mbisa akiri

Mussa Mbissa Golikipa Musa Mbissa

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: Mwananspoti

Katibu Mkuu wa Tanzania Prisons, Anthony Hau amesema wamekubaliana na uamuzi uliotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuwafungia kusajili kwa dirisha moja.

Prisons ilikutwa na makosa ya kumsajili, Kipa Musa Mbissa aliyekuwa na mkataba na Coastal Union kama ilivyo kwa Singida Big Stars iliyomsajili, Metacha Mnata aliyekuwa Polisi Tanzania.

Hau alisema licha ya kujitetea lakini walikutwa na makosa na sasa watahakikisha benchi la ufundi likitumia wachezaji waliopo kuzidi kuimarisha kikosi chao.

“Wachezaji wengi wa Tanzania wamekuwa sio wa kweli kwenye mambo ya mikataba, kama utakumbuka msimu uliopita tulikuwa na hali mbaya kwenye ligi na tuliweka nguvu nyingi kuhakikisha tunabaki Ligi Kuu.

“Wenzetu wakati wanaendelea na usajili sisi tulikuwa na michezo ya mtoano na mambo mengi tuliyaacha kuhakikisha tunafanya vizuri michezo ya mwisho,” alisema Hau.

Aliongeza wakati wanaanza kusajili zilisalia wiki mbili hivyo muda haukuwa rafiki kwao na walijitahidi kukimbizana na muda ili dirisha la usajili linapofungwa wawe wamemaliza kusajili wachezaji.

Hau alisema kuna wachezaji usajili wao haukukamilika licha ya mambo mengine kwenda sawa na uongozi ulipanga kukamilisha hilo dirisha dogo la usajili lakini kwa sasa wamekwama.

Kwa upande wake Mbissa alisema “Nipo kwenye mazungumzo na msimamizi wangu kulifuatilia zaidi, lakini ni kweli mkataba wangu ulikuwa bado haujaisha japokuwa kulikuwa na kipengele cha makubaliano kwamba nikipata timu naweza kuondoka,” alisema kipa huyo.

Chanzo: Mwananspoti