Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons ruksa kusajili, Mgunda apiga 'hat-trick' ASFC

Mgunda Hat Trick.jpeg Mshambuliaji Ismail Mgunda wa Tanzania Prisons akipokea mpira wake baada ya kufunga mabao matatu

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) limeiondolea adhabu Tanzania Prisons ya kutosajili kwa kipindi cha dirisha dogo badala yake itapaswa kulipa sh1 milioni kabla ya dirisha kufunguliwa.

Prisons ilikutana na rungu hilo awali baada ya kubainika kumsajili aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Mussa Mbisa aliyekuwa na mkataba sawa na Singida Big Stars waliokuwa wamemsajili aliyekuwa kipa wa Polisi Tanzania, Metacha Mnata na sasa timu hizo tayari zimefutiwa adhabu hiyo na zitapaswa kulipa faini ya Sh1 milioni kabla ya dirisha kufunguliwa, Desemba 15.

Katika taarifa iliyotolewa leo Desemba 11 imeeleza kuwa kamati imesikiliza mapitio yaliyowasilishwa na Tanzania Prisons kuhusu uamuzi wa awali kufungiwa kusajili kwa kipindi cha dirisha dogo.

"Baada ya kupitia hoja, klabu yako imeondolewa adhabu ya kufungiwa kusajili kwa dirisha dogo badala yake imepigwa faini ya Sh1 milioni ambayo inapaswa kulipwa kabla ya dirisha kufunguliwa," imesema taarifa hiyo.

Akizungumzia uamuzi huo, katibu mkuu wa Tanzania Prisons, Anthony Hau amekiri kupokea barua kutoka TFF ikiwa ni majibu ya maombi yao waliyowasilisha.

Amesema baada ya kuruhusiwa kusajili wanasubiri ripoti ya benchi la ufundi kujua wanahitaji kuongeza wachezaji wangapi kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mzunguko wa pili.

"Tunashukuru sana kamati kwa uamuzi wa busara kwetu, tayari Coastal Union tumeanza kuwalipa stahiki yao ili kipa aendelee kuwa mali yetu halali, tunasubiri kocha mkuu, Patrick Odhiambo atupe ripoti, uongozi unapambana hadi kufikia Alhamisi tuwe tumelipa faini hiyo," amesema Hau.

Katika hatua nyingine, timu hiyo imefuzu hatua ya 32 ya michuano ya kombe la shirikisho (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Misitu FC ya mkoani Tanga.

Katika mchezo huo uliopigwa leo uwanja wa Sokoine jijini hapa, mchezaji Ismail Mgunda ameondoka na mpira baada ya kufunga mabao matatu 'hat-trick', huku mengine yakifungwa na Joshua Nyantin aliyeweka mawili sawa na Zabona Hamis, huku la Misitu FC likiwekwa na Saleh Sazui.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live