Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons mzuka kama wote

Prisons Pic Data Prisons mzuka kama wote

Tue, 30 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

BAADA ya mapumziko mafupi mastaa wa Tanzania Prisons, leo wanarejea tena kambini kujiandaa na mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, huku kocha wa timu hiyo Shaaban Kazumba akisisitiza anataka vijana wao waendelee na kasi ile ile waliyokuwa nayo kabla ligi haijasimama.

Prisons imeonekana moto baada ya kucheza mechi sita mfululizo bila kupoteza hata mmoja, huku ikizibana timu kubwa na kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kazumba aliliambia Mwanaspoti kuwa leo nyota wake wanarejea tena kambini kuanza maandalizi ya mashindano yao huku akitamba kuwa moto wao hauzimiki.

Alisema kwa sasa wanasubiri ratiba mpya kutokana na msiba mzito ulioikumba Taifa kwa kuondokewa na aliyekuwa Rais, Hayati John Magufuli na kwamba Prisons wako tayari kwa kila kitu.

“Hatujajua kama tutaanza na Yanga mechi ya FA au Polisi Tanzania kwenye ligi, lakini niseme sisi tutakuwa tayari kwa ratiba yoyote na tunapoanza kambi programu ni zilezile zilizotupa mafanikio,” alisema Kazumba.

Kocha huyo aliongeza pamoja na matokeo mazuri waliyonayo lakini hawawezi kuridhika isipokuwa lazima waweke mipango sawa ili kuendeleza rekodi nzuri na kumaliza nafasi nne za juu.

Alisema kipindi kama hiki timu nyingi zinafanya maandalizi kabambe kwa lengo la kupambania nafasi za juu lakini nyingine zikichuana vikali kukwepa kushuka daraja hivyo wao watakomaa kusaka ushindi kila mechi.

“Hata sisi tunatamani zile nafasi tatu za juu ili ikitokea fursa ya kuwakilisha kimataifa tunaenda, kwa sasa timu zimejipanga kujinusuru kushuka daraja kwahiyo lazima Prisons tuwe makini,” alisema Kazumba.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz