Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons kusajili mshambuliaji wa Ukraine

Prison Ukraine Prisons kusajili mshambuliaji wa Ukraine

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa klabu ya Tanzania Prisons upo kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji Yohana Mkomola aliyekuwa anacheza soka la kulipwa katika klabu ya Vorskla Poltava inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ukraine.

Mkomola aliachana na timu hiyo baada ya kutokea machafuko ya amani nchini humo na Shirikisho la soka la kimataifa (Fifa) lilitoa vibali vya timu zote za Ukraine zenye wachezaji wa kigeni kuwaruhusu watafute timu nyingine ili kulinda vipaji vyao.

Baada ya mabosi wa Prisons kupata taarifa mchezaji huyo yupo huru hadi sasa na wanataka kuboresha kikosi chao, tayari wameshafanya mazungumzo na wamekubaliana kila kitu na kilichobaki ni mchezaji huyo aweke saini ya kuitumikia timu hiyo kwa miezi sita.

Mmoja wa viongozi kutoka ndani ya Prisons alilidokeza Mwanaspoti tayari wameshafanya mazungumzo na Mkomola na kilichobaki ni kusaini tu muda wowote baada ya mchezaji kupata barua kutoka chama cha soka cha Ukraine.

“Tayari mazungumzo yameshafanyika kwa kiasi kikubwa na kuna baadhi ya vitu vikikamilika atajiunga na sisi labda kama litatokea jingine,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;

“Tunataka tuboreshe kwenye eneo letu la ushambuliaji ili tufanye vizuri katika mzunguko huu wa pili.”

Upande wa Yohana alipofutwa alijibu kwa kifupi;”Nitarudi uwanjani siku sio nyingi, nitakuwa wapi subilini mtaona.”

Mshambuliaji huyu kabla ya kwenda nje ya nchi alicheza katika kikosi cha Yanga na alitolewa kwa mkopo kwenye timu ya African Lyon lakini hakucheza badala yake aliondoka na kwenda Ukraine.

Wakati huo huo kiungo mkongwe Mwinyi Kazimoto inaelezwa yupo kwenye mazoezi na timu ya Ruvu Shooting yaliyofanyika jana huku ikidaiwa wanataka kumsajili ili aongeze nguvu katika kikosi chao.

Mmoja wa viongozi wa juu kwenye timu ya Ruvu Shooting alisema kwa kifupi;”Mwinyi yupo huku na kocha anamuangalia,akishawishi benchi la ufundi atachukuliwa.”

Chanzo: Mwanaspoti