Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons, Tabora vita ya mabao, rekodi

Tabora United Www Prisons, Tabora vita ya mabao, rekodi

Wed, 28 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Tanzania Prisons ikiahidi kulipa kisasi, Tabora United wamesema hawakubali tena kupoteza pointi yoyote ili kujinasua nafasi za chini kwenye Ligi Kuu.

Timu hizo zinatarajia kukutana kesho Jumatano katika Uwanja wa Sokoine mchezo utakaopigwa saa 8 mchana ukiwa wa raundi ya 18 kwenye Ligi Kuu, huku kila timu ikijivunia rekodi zake.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Tabora United ikiwa nyumbani Ali Hassan Mwinyi ilishinda mabao 3-1 na kesho itakuwa vita ya kisasi au rekodi kwa wapinzani hao.

Tabora United haijashinda katika michezo saba ya mwisho na imekuwa ikiambulia sare nne dhidi ya Mashujaa, Namungo, Azam na Singida FG na vipigo vitatu dhidi ya Ihefu 2-1, Yanga 1-0 na Simba 4-0 huku ikishinda 2-1 Desemba 1 2023 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hadi sasa Prisons wapo nafasi ya saba kwa pointi 21, huku Tabora United wakiwa nafasi ya 12 kwa alama 18 baada ya timu zote kushuka uwanjani mara 17 na kufanya mechi ya leo kuwa ya vita kali.

Katika michezo minne kwa timu hizo, kila upande umeruhusu mabao ambapo Prisons wavu wao umeguswa mara nne na kufunga sita, huku Tabora United wakifunga mawili na kuruhusu sita.

Nahodha msaidizi wa Prisons, Khamis Mcha alisema mchezo huo wanahitaji kulipa kisasi akieleza kuwa katika mechi zilizopita wamekuwa wakiruhusu mabao ya haraka, ishu ambayo hawataki kujirudia leo.

“Pamoja na matokeo mazuri kwetu, lakini hatuwezi kuwadharau wapinzani na tunahitaji kulipa kisasi, tumeruhusu bao takribani kila mechi lakini hatutaki ijirudie,” alisema Mcha.

Kwa upande wake beki wa Tabora United, Shafii Maulid alisema baada ya kukosa ushindi katika mechi saba mfululizo, hivyo wanaenda kuanza na Prisons na hawatakubali kuruhusu bao la mapema.

Chanzo: Mwanaspoti