Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons, Mashujaa vita ya ndugu

Prisons Pcers Prisons, Mashujaa vita ya ndugu

Sun, 19 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Mashujaa ikipigia hesabu za pointi tatu leo, wapinzani wao Prisons wamesema hawakubali tena kukosa ushindi ili kurejesha furaha kwa mashabiki ikiwa ni mechi ya mwisho nyumbani.

Mashujaa iliyo nafasi ya 13 na pointi 26, itaikabili Prisons iliyo nafasi ya tano na pointi 33 kwenye Uwanja wa Sokoine, ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu raundi ya 28.

Mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Prisons nyumbani, kwani baada ya dakika 90 itasafiri kukipiga dhidi ya Namungo na kuhitimisha msimu mbele ya Yanga, Mei 28.

Timu hizo zinakutana Prisons ikikumbuka ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na mchezo wa leo utakuwa ni kisasi na rekodi, ingawa kila moja inasaka ushindi ili kujiweka pazuri.

Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdalah Mohamed ‘Baresi’ alisema wanafahamu ugumu na umuhimu wa mechi hiyo, hivyo kazi itakuwa moja tu, kutafuta ushindi na si vinginevyo.

“Vijana wanajua tunaenda kufanya nini, hatuhitaji matokeo mengine zaidi ya pointi tatu, hivyo tusubiri dakika 90 zitaamua,” alisema kocha huyo aliyewahi kuinoa Prisons.

Kocha Mkuu wa Prisons, Ahmad Ally alisema baada ya kukosa ushindi katika mechi nane mfululizo, leo ndio sehemu ya kukata kiu na liwake jua, inyeshe mvua, lazima kieleweke.

“Ndiyo mechi ya mwisho kucheza nyumbani msimu huu, lazima tuwape furaha mashabiki, tunajua wapinzani walipandia hapa Sokoine, lakini tunachotaka ni ushindi ili kuwa salama,” alisema kocha huyo.

Chanzo: Mwanaspoti