Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons, Dodoma wako live

Dodoma Live Prisons, Dodoma wako live

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kukabidhiwa jukumu kuinoa Tanzania Prisons, Kocha mkuu wa timu hiyo, Ahmad Ally leo Jumatano ataanza kibarua chake kuikabili Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Ally ambaye alichukua mikoba ya mtangulizi wake, Fredi Felix ‘Minziro’, utakuwa mchezo wake wa kwanza baada ya ule uliopita dhidi ya Coastal Union kuishia jukwaani.

Kocha huyo alisema anafahamu mtihani alionao akiahidi kufanya vizuri, huku akieleza kurejea kwa baadhi ya nyota wake akiwamo Edwine Balua, Jeremia Juma na Jumanne Elfadhir.

Alisema Dodoma Jiji wamekuwa na mwendelezo mzuri wa Ligi Kuu, lakini lolote linaweza kutokea kutokana na maandalizi waliyoyafanya tangu akabidhiwe kibarua hicho.

“Mechi iliyopita nilifuatilia kujua makosa yalipo na nimeweza kufanya nao mazoezi na kurekebisha mapungufu hivyo naamini tunaweza kupata ushindi na kujinasua nafasi za chini,” alisema Kocha huyo.

Nyota wa timu hiyo, Hamis Mcha alisema pamoja na matokeo waliyonayo lakini muda utafika wataondokana na upepo huo mbaya na Prisons itaanza kufanya vizuri na kumaliza ligi nafasi za juu.

“Kimsingi hakuna anayefurahia hali hii kwa wachezaji tunajua maumivu ya mashabiki waliyonayo kuhusu matokeo haya, ila tunaamini muda utafika timu itakaa sawa na tutaanza kumpiga yeyote,” alisema kiungo huyo mkabaji.

Kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope alisema wanaingia uwanjani kwa tahadhari na umakini wakiwaheshimu wapinzani bila kujali matokeo waliyonayo.

“Kucheza na timu iliyo chini inakuwa ngumu kuliko iliyopo juu, lazima tuwaheshimu Prisons kutokana na mpira walionao muda wote, tumesafiri na kikosi kamili tukihitaji pointi tatu,” alisema Liogope.

Timu hizo zinakutana ikiwa Prisons yupo nafasi ya 15 kwa pointi saba baada ya kushinda mchezo mmoja, huku Dodoma Jiji wakiwa nafasi ya sita kwa alama 15 baada ya mechi 10 kwa kila upande.

Chanzo: Mwanaspoti