Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prince Dube hauzwi Sh800 milioni

Prince MPUMELELO DUBE Prince Dube

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna mchezaji Tanzania nzima ambaye anaweza kuwa na thamani ya Sh800 milioni. Hakuna. Nimeshtuka baada ya kuambiwa kuwa thamani ya mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube ni zaidi ya Sh800 milioni.

Ni kweli tuna wachezaji wengi mastaa kwa sasa nchini na mwana wa Mfalme, Prince Dübe akiwemo. Ni mchezaji wa daraja la juu kwenye ligi yetu, lakini ukiniuliza kiukweli hawezi kuwa na thamani hiyo.

Tatizo la mpira wetu mchezaji anaweza kupewa tu thamani mezani. Viongozi wetu bado hawaamini kuwa biashara ya wachezaji ni kubwa sana dunaiani. Bado wanaweka bei kubwa kwenye mikataba ya wachezaji ili kuzuia timu inayomtaka mchezaji ishindwe kumnasa.

Hili ndilo tatizo mama ninaloliona. Kuanzia kwa Feisal Salum, Stephane Aziz KI, Clatous Chama hakuna hata mmoja ambaye anatakiwa kufikisha thamani ya Sh800 milioni. Kiukweli simuoni.

Mchukue Maxi Nzengeli, Kibu Dennis, Pacôme Zouzoua sioni anayeweza kuwa na thamani ya milioni 800. Wachezaji wengi Tanzania wana thamani za kubumba tu kwenye mikataba yao.

Nimeshangaa sana kuambiwa Prince Dube ana thamani ya milioni 800. Kiukweli Tanzania kwa sasa sioni mchezaji mwenye thamani hiyo. Simuoni Simba. Simuoni Yanga. Siku klabu zetu zikigundua kuwa kuuza na kununua wachezaji ni biashara nzuri duniani, wataanza kufungua milango ya wachezaji kutoka klabu moja na kwenda nyingine.

Mikataba mingi ya wachezaji wetu imewekwa thamani kubwa ili kuzuia mchezaji kuondoka. Ni lazima tutoke huko. Hilo ni soka la kizamani. Dunia ya leo mambo yamebadilika. Mpira ni biashara kubwa duniani.

Kumekuwa na tetesi za Klabu ya Yanga kumtaka Prince Dube ingawa hakuna mawasiliano rasmi yanayoendelea. Dube amefika mahali amewaaga kabisa viongozi, wachezaji na mashabiki wa Klabu ya Azam kuwa anaondoka. Amechoshwa na maisha tena ya waoka mikate wa jiji la Dar es Salaam.

Siyo jambo la kufurahia hata kidogo maana sakata hili ni kama lile la Feisal Salum na Klabu ya Yanga ambalo kimsingi, Feisal hakuwa na haki ya kuvunja mkataba. Ule ni uhuni uliofanyika. Ni kama hiki kinachoendelea cha Prince Dube na Klabu ya Azam.

Dube hana sababu za msingi zinazomfanya atake kuondoka ndani ya Klabu ya Azam. Ni uswahili tu. Kutaka kuondoka katikati ya msimu ni utoto. Azam FC wanampa kila kitu ambacho anakitaka sema mwana wa mfalme ameshikwa masikio mahali. Amekuwa mswahili.

Fifa ina taratibu zake za wachezaji kuhama klabu moja na kwenda nyingine. Hakuna hata moja ambayo inambeba Prince Dube. Lakini hilo tukiliweka pembeni, ni kweli thamani ya Dube ni zaidi ya Sh800 milioni za Kitanzania? Jibu langu ni hapana.

Dube hawezi kuwa na thamani hiyo. Ni kweli kwamba ni mshambuliaji mzuri, lakini hawezi kufikisha thamani hiyo. Wachezaji wetu ni lazima waamke. Mara nyingi sana thamani ya mchezaji kuondoka klabuni hapa kwetu wanaoamua ni viongozi wa klabu bila hata mchezaji mwenyewe kuhusika. Sidhani kama iko sawa.

Ni lazima mchezaji na uongozi ukae chini na kujadili kwa pamoja. Prince Dube ni mchezaji mzuri, lakini thamani yake haiwezi kuwa zaidi ya Sh800 milioni.

Mojawapo kati ya vitu ambavyo huongeza thamani kwa mchezaji ni nafasi anayocheza. Duniani kote wachezaji wenye thamani ya juu ni washambuliaji na kwa hili Dube pia ni mshambuliaji.

Lakini wenzetu wanakwenda mbele na kuangalia uwezo wake kama mshambuliaji. Prince Dube ana msimu wa nne sasa ndani ya Ligi Kuu Bara na hajawahi hata msimu mmoja kuwa mfungaji bora. Dube pamoja na kuwa ni mshambuliaji mzuri, lakini rekodi yake ya kuumia kila msimu inapunguza sana thamani yake.

Dube hajawahi kuwa mchezaji bora hata msimu mmoja. Haya mambo huwa yanachangia mchezaji thamani yake kuongezeka. Jambo lingine huwa ni umri. Dube ana miaka 27 sasa. Sio mtoto tena. Yuko kwenye umri wa kushinda mataji. Pale Azam FC hajashinda taji lolote kubwa.

Ukitazama uwezo wake kwenye mechi za kimataifa bado ni kawaida sana. Hawezi kuwa mchezaji mwenye thamani ya Sh800 milioni. Azam FC imekuwa ikitolewa kila mara katika mashindano ya klabu Afrika na yeye akiwemo kwenye hatua za awali kabisa.

Sikatai ni mchezaji mzuri, lakini bado hana thamani hiyo. Kitu kingine mabacho huongeza thamani ya mchezaji ni mafanikio yake ya timu ya taifa. Ni kweli Dube anaitwa mara kwa mara kwenye timu yake ya taifa, Zimbabwe, lakini hajawahi kuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza.

Hakuna Mafanikio makubwa aliyopata akiwa timu ya taifa mbali na kushiriki tu michuano ya Afcon. Bado Dube hawezi kuwa na thamani kubwa kiasi hicho. Kuna haja ya wachezaji wetu kuamka kwenye makubaliano ya kimkataba.

Ni lazima wapata nafasi ya kujadili vipengele hasa vinavyohusu kuondoka kwao. Ni lazima pia wachezaji wawe waungwana maana naona mtindo anaotaka kuondoka nao Dube pale Azam FC ni mtindo wa mtaani. Ni usela tu.

Najaribu pia kutazama nafasi ya Dube pale Jangwani kama tetesi zinavyosema. Yanga ya sasa si nyepesi. Kama Dube ataelekea Yanga, inabidi aende kukaza sana. Dube bado hajathibitisha kukupa mabao 10 ya ligi kwa msimu. Dube bado hajathibitisha kuwa fiti msimu mzima.

Malengo ya Azam FC kwa msimu ni tofauti sana na Yanga. Presha ya Klabu ya Azam ni tofauti sana na Yanga. Yanga ni dude kubwa sana nchini. Ushindani pale Yanga wa mataji na nafasi ya kucheza ni mkubwa kuliko Klabu ya Azam. Mbaya zaidi, Yanga hawana muda wa kupoteza. Wanataka kila msimu ubingwa wa ndani. Wanataka kila msimu kufanya vizuri kimataifa.

Tayari ukiitazama Yanga chini ya Kocha Gamondi, inategemea zaidi mabao kutoka kwa viungo washambuliaji. Hakuna mtu maalumu mwenye jukumu la kufunga. Price Dube kama anakwenda Jangwani ni lazima kocha abadili mfumo wa ushambuliaji ili kuweza kumfanya Dube aingie ndani.

Yanga ni kubwa sana kwa Dube. Kuna vitu vingi lazima apambane ili akatimize malengo yake na yale ya timu. Amekuwa mzuri sana kwenye mechi kubwa, lakini Yanga itakuwa ni habari nyingine. Kila kitu ni tofauti na Azam FC. Yanga inaweza kucheza bila mshambuliaji wa asili na ikafanya kweli.

Yanga hawana pia uvumilivu mkubwa. Ni mtu kazi kwelikweli. Kama Dube atakuwa fiti na kocha akamjengea uwezo, anaweza kwenda kuwa mchezaji mkubwa zaidi. Lakini pamoja na yote, bado simuoni Dube kama mchezaji mwenye thamani ya Sh800 milioni.

Chanzo: Mwanaspoti