Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prince Dube apeleka staili tano Yanga

PRINCE DUBE MSH Prince Dube

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ndo hivyo, Prince Dube anahusishwa na mpango wa kuhamia Yanga. Hali ilivyo, fowadi huyo wa kimataifa wa Zimbambwe ataachana na klabu yake ya sasa ya Azam FC baada ya kuandika barua ya kuomba kuachwa na miamba hiyo Chamazi huku pia akiandika ujumbe wa Instagram kuaga mashabiki na uongozi.

Yanga inaonekana ni kama ni kituo kinachofuata kwa Dube atakapomalizana na maisha ya Azam Complex. Kama Dube atafanikiwa kukamilisha dili hilo la kwenda Yanga, basi atakuwa amefuata nyayo za Wazimbabwe wenzake, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko waliocheza kwa mafanikio makubwa walipokuwa kwenye kikosi hicho chenye makazi yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.

Kwa sasa, mashabiki wa Yanga wanaanza kuvuta hisia namna timu yao itakavyokuwa wakati Dube atakapotua rasmi kwenye kikosi cha timu hiyo ya Wananchi. Kama hilo likifanikiwa, jambo hilo litakwenda kushuhudia mastaa kibao wakipoteza nafasi zao kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Miguel Gamondi.

Mwanaspoti linatazama njia tofauti ambazo Gamondi anaweza kumtumia Dube kwenye safu ya ushambuliaji ya timu yake kwenye msimu wa 2024/25.

4-2-3-1; Dube straika

Sehemu kubwa ya msimu huu, kocha Gamondi amekuwa akitumia fomesheni ya 4-2-3-1, kutoa nafasi kwa viungo wake washambuliaji watatu, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki kuanza kwa pamoja, wakicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati, ambapo amekuwa akiwabadili, kama si Clement Mzize basi atakuwa Kennedy Musonda au Joseph Guede.

Lakini, ujio wa Dube utakwenda kuleta mabadiliko kwenye eneo hilo la mshambuliaji wa kati, ambapo kocha Gamondi anaweza kwenda kuanza naye moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza hasa baada ya kuthibitisha kwamba kuna kitu amekuwa akikifanya kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Kwa maana hiyo, kwenye mfumo huo wa 4-2-3-1, Musonda, Mzize na Guede watampisha Dube.

4-3-3; Dube kulia

Uwezo wa Dube wa kushambulia kutokea pembeni, akifanya vyema kwenye nafasi ya Namba 9 bandia, hilo linaweza kumfanya kocha Gamondi akashawishika kutumia fomesheni ya 4-3-3. Gamondi anaweza kuchagua mfumo huo kwenye mechi ambazo atahitaji kikosi chake kuwa kwenye umiliki wa mpira muda mwingi ambapo atahakikisha anakuwa na viungo wenye uwezo mkubwa wa kutulia na mipira kwenye miguu yao. Katika mtindo huo wa kiuchezaji, safu ya mabeki wanne inaweza kuundwa na Joyce Lomalisa, Dickson Job, Ibrahim Bacca na Kouassi Attohoula Yao, ambapo kwenye mstari wa viungo watatu wa kati, utakuwa na Khalid Aucho, Mudathir Yahya na Pacome, wakati mbele, Dube atacheza upande wa kulia, Aziz Ki na Maxi kwenye upande wa kushoto. Dube ameonyesha uwezo wa kufunga hata akishambulia kutokea kulia.

3-4-3; Dube kushoto

Gamondi amebahatika kuwa na kikosi chenye mabeki wa kati wenye uwezo mkubwa, ambao wanamruhusu kucheza fomesheni ya 3-4-3 kwa maana ya kutumia mabeki wa kati watatu bila ya matatizo yoyote. Gamondi anaweza kuanza na ukuta wa mabeki wa kati, Job, Bakari Mwamnyeto na Barca. Kingine, Gamondi amebahatika pia kuwa na wing-back mahiri kama Yao kwenye upande wa kulia na Nickson Kibabage ay Lomalisa Mutambala kwenye upande wa kushoto, ambao watasimama kwenye mstari wa kati sambamba na viungo wa kati, Aucho na Mudathir Yahya. Kwenye mstari wa wakali watatu watakaocheza mbele, Dube atashambulia kutokea upande wa kushoto, ambako amekuwa tishio sana kutokana kutumia mguu wa kulia na uwezo wake kufunga kwa mashuti ya mbali. Hapo atacheza sambamba na viungo wa ushambuliaji Aziz Ki na Pacome.

4-1-4-1; Dube kwenye boksi

Huu ni mfumo unaohitaji nidhamu kubwa kwenye kukaba kwa umoja ili kumsaidia kiungo mkabaji, ambaye atakuwa amesimama peke yake, asizidiwe na wapinzani, endapo kama wataweka watu wengi eneo hilo na wenye uwezo wa kutulia na mipira kwenye miguu yao. Lakini, fomesheni hiyo ya 4-1-4-1 inatoa nafasi ya kukabia juu, huku mshambuliaji wa kati, ambaye ni Dube atakuwa amesimama kwenye boksi kuhakikisha mabeki wa kati wa timu pinzani wanabaki kwenye eneo hilo, kuwapunguzia idadi ya namba ndani ya uwanja. Kwenye mstari wa wachezaji wanne nyuma ya mshambuliaji wa kati, patakuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kukaa na mipira kama Maxi, Aziz Ki, Mudathir na Pacome. Kwenye mfumo huo, Sure Boy au Farid Musa anaweza kutumika pia kwenye huo mstari wa mastaa wanne nyuma ya Dube.

4-4-2; Dube na Musonda mbele

Gamondi anaweza kuchagua kutumia fomesheni ya 4-4-2 (Diamond), ambapo mmoja kati ya Pacome na Aziz Ki anaweza kuanzia benchi ili kutoa nafasi kwa Musonda kucheza sambamba na Dube kwenye safu ya ushambuliaji. Kwenye fomesheni hiyo, safu ya mabeki inaweza kubaki vilevile ya wakali wanne, Lomalisa, Job, Bacca na Yao, huku kwenye kiungo kunaweza kuwa na huduma ya Maxi, Aucho, Muda na Pacome au Aziz Ki, ili Musonda na Dube wacheze kwenye eneo la mbele. Kwa sababu, Dube ni mshambuliaji asiyeweza kutulia sehemu moja, kwenye mtindo huo anaweza kucheza pia na ama Mzize au Guede.

Chanzo: Mwanaspoti