Sakata la mshambuliaji Prince Dube limeingia sura mpya baada ya nyota huyo raia wa Zimbabwe kudai ndani ya klabu ya Azam viongozi wa klabu hiyo hufurahia mafanikio ya timu zingine badala ya timu yao.
Dube ambaye ameshaondoka ndani ya Azam FC, amesema kuwa wakati anajiunga na klabu hiyo alidhani kuwa ni timu kubwa na pengine ingemsaidia kupambana kukuza wasifu wake na kuipa mataji timu lakini ameambulia kushuka wasifu wake tofauti na alivyokuja huku akiwalaumu viongozi wa timu hiyo kuwa hawana malengo ya kushinda mataji.
“Kama nilivyosema nilipokuja hapa nilikuwa na malengo na matumaini kwa timu nilidhani kua ni timu kubwa ambayo ingeweza kushindana na wasifu wangu ungeongezeka zaidi.
“Wasifu wangu ulianza kushuka niliendelea kujisemea kua mambo yatakuwa mazuri lakini kila mara mambo yalikua yanaenda kuwa mabaya zaidi, unaweza kuona tunaanza msimu vizuri lakini katikati kila kitu kinakuwa kama misimu iliyopita.
“Sikutaka kusema lakini imefika muda inanibidi tu niseme, ndani ya timu kuna watu tena viongozi wa juu walikua wakituhujumu. Haiwezekani viongozi wa ngazi za juu Wanakatwa wanashabikia timu zingine tena bila hata kujificha, timu zingine zikishinda wanafurahia.
“Ndiyo maana nataka mabadiliko, nahitaji kuchezea timu ambayo wachezaji na viongozi wana lengo moja. Viongozi wako Azam, lakini mioyo yao iko kwenye timu zingine wanazozisapoti, hili ni tatizo jingine.
"Kwenye timu mnaanza msimu matumaini yakiwa makubwa lakini mnaanza kupoteza na hakuna anaejali, natamani kupata changamoto mpya kwenye mazingira mapya kujaribu vitu vingine, kucheza sehemu yenye pressure kubwa na kuona namna mambo yanavyo kwenda mbele.
“Siwezi kuwa kwenye timu ambayo wewe unataka kushinda kitu lakini watu ambao wanawaongoza wanasapoti timu mnayoshindana nayo, ndiyo maana nataka mabadiliko niwe sehemu ambayo watu wanaowaongoza mnafikiria kitu kimoja.
“Kama mchezaji unahitaji kushinda makombe, unatamani kushindana, dhamira yangu ni kucheza ndani ya Africa na Ulaya,” amesema Dube.