Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Presha imepanda Simba, Yanga

Vigogo Presha Presha imepanda Simba, Yanga

Wed, 27 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Pesa tamu. Klabu nane zilizopo kwenye hatua ya nane bora ya Ligi Mabingwa Afrika tayari zina uhakika wa Sh2.2 bilioni. Sasa kila mmoja anapambana kusaka Sh3 bilioni na ushee za nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika.

Wageni wawili ambao muda wowote wanaweza kukanyaga kwenye ardhi ya Tanzania kucheza karata zao za kwanza mbele ya Simba na Yanga presha zimewapanda.

Siyo Al Ahly ambaye ni bingwa mtetezi wala Mamelodi wenye utajiri mkubwa, wote presha ziko juu na kila mmoja amezungumza na Mwanaspoti na kueleza ugumu wa mchezo huo wa Dar es Salaam ambao utatoa picha halisi.

AHLY WALIA NA BENCHIKHA

Simba ilirejea jijini Dar es Salaam jana mchana baada ya kujichimbia visiwani Zanzibar kwa wiki moja ikijifua kwa siri na mazoezi makali lakini ilipotua tu ikakuta wageni wao Al Ahly nao watu wao wameshatua mjini siku moja nyuma yao, ila wakimtaja kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha.

Ahly ambayo kikosi chake kitatua nchini leo na ndege ya shirika la nchi yao ya Misri, imemtanguliza kiungo wa zamani Hossam Ghally akiwa ndiye mkuu wa msafara wa Waarabu hao ambaye mwaka 2016, aliwahi kudhalilishwa na kiungo wa Simba, Clatous Chama.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ghaly ambaye ni kati ya wakongwe wanaoheshika wa timu hiyo alisema hawana wasiwasi sana na ubora wa kikosi cha Simba, lakini kama ukitokea ugumu basi utasabishwa na kocha Benchikha ambaye kwao ndiye kizuizi kutokana na aina ya mikakati yake kwenye mechi za namna hiyo.

Ghaly alisema mechi yao ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa itakuwa ngumu kutokana na rekodi ya Benchikha ambaye kila walipokutana naye amekuwa akiwapa ugumu kutokana na kujua kucheza kwa mkakati na ni kocha mzuri wa mechi za mtoano tangu akiwa na timu za Uarabuni.

Hata hivyo, staa huyo ambaye amewahi kuzitumikia Feyenoord ya Uholanzi na Tottenham Hotspur ya England, alidai kwamba Ahly bado ina nafasi ya kutumia uzoefu wake kutinga nusu fainali.

Kauli hiyo ya Ghaly inaweka wazi juu ya Waarabu hao wanavyokumbuka jinsi kocha huyo Mualgeria alipowashangaza akiwachapa kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa Super Cup uliowakutanisha bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, USM Alger dhidi ya bingwa wa Ligi ya Mabingwa, Ahly.

“Simba tunaweza kuifunga, lakini nadhani kitu kinachotufanya tuwe makini ni uwepo wa kocha Benchikha (Abdelhak). Nadhani mnafahamu ubora wa huyu kocha kwa sasa na namna anavyojua kusimama na mbinu zake,” alisema Ghaly ambaye Chama aliwahi kumtesa alipokuwa na Zesco mwaka 2016 - Ahly ikilala kwa mabao 3-2 na kutupwa nje ya mashindano hayo kwenye hatua ya robo fainali.

“Nipo hapa kuhakikisha timu inapata wakati mzuri wa mechi hii ya Ijumaa (Machi 29). Tunaamini makocha wetu watakuja na mpango mzuri wa kushinda, hatujawahi kupata ushindi hapa kwa Mkapa na Simba hili ni eneo lingine ambalo linatufanya kuwa makini na mechi hii.

“Sina wasiwasi na kikosi chetu tutacheza kwa ubora wetu kupata matokeo mazuri ambayo yatatupa wepesi kabla ya mechi ya marudiano kule Cairo. tunataka kutetea ubingwa wetu.”

Benchikha anasifika kwa kujua kusimamia ajenda moja mpaka timu ifanikiwe akiwa amewahi kufanya hivyo RB Berkane ya Morocco na USM Alger kisha zote akazipa makombe ya Shirikisho Afrika.

Simba kama ilivyoondoka ikiwa kimyakimya jana pia imerejea kiimyakimya huku Mwanaspoti likifahamu kuwa ni mkakati wa Benchikha aliyemzuia yeyote kuzungumzia maandalizi yao wala kilichofanyika kambini kwao akigoma kurekodiwa kitu chochote zaidi ya picha za mnato.

Simba na Ahly zimeshacheza michezo minane, kila moja imeshinda nyumbani kwake michezo mitatu zikitoka sare kwenye michezo miwili, mmoja Dar es Salaam na mmoja Cairo - Misri.

Hata hivyo, kwenye Ligi ya Mabingwa hivi karibuni, mchezo huu ndiyo unatazamwa kwa umakini wa hali ya juu kwa kuwa ni mara ya kwanza timu hizo zinakutana kwenye mtoano mechi nyingine zote zimekutana katika hatua ya makundi.

Mchezaji Luis Misquissone anaweza kuiongozea Simba maujanja ya Ahly kwa kuwa miaka ya hivi karibuni alitoka kwenye timu hiyo na kurejea Msimbazi.

Asilimia kuwa ya wachezaji wa Ahly wanamfahamu vizuri staa huyo raia wa Msumbiji, kama ambavyo anaifahamu Ahly nje ndani.

KOCHA MAMELODI ATAJA KIZUIZI

Wakati Yanga ikiendelea na maandalizi tayari kwa kukutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, kocha wao amesisitiza kwamba wanatakiwa kuchukua tahadhari juu ya mchezo huo kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji ndani ya kikosi hicho.

Mokwena aliongeza kuwa ubora wa wachezaji wa Yanga na wale wa Mamelodi utakuwa na nguvu kubwa ya kuamua mchezo huo utakaopigwa Jumamosi, Machi 30, Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 3:00 usiku.

Mokwena alisema timu yake inajiandaa kupata ushindi mbele ya Yanga, lakini tahadhari yao nyingine ukiacha mastaa wenye uzoefu ni uwepo wa kocha Miguel Gamondi ambaye anajua karibu falsafa nzima ya klabu yao kwa kuwa aliwahi kufanya kazi hapo.

“Tunahitaji kushinda, tunajipanga kufanya hivyo hatutaangalia ukubwa wa jina letu tunataka ubora uamue mchezo. Haitakuwa mechi rahisi kwa pande zote. Tunawaheshimu Yanga wako chini ya kocha anayeijua Mamelodi Gamondi ni kocha mkubwa,” alisema Mokwena.

“Sisi tunajipanga kukutana na Yanga bila kuangalia kuna mchezaji gani hayupo au yupo tunajiandaa kukutana na Yanga iliyo kamili na kwa ubora wao.”

Wakati Mokwena akiyasema hayo mchambuzi maarufu wa soka kutoka Ivory Coast, Mamadou Gaye amewaonya Mamelodi kutowafuata Yanga kwa mazoea kwani wanaweza kujikuta wanashangazwa.

Gaye akizungumza kwenye kipindi cha ‘Pithside kinachoendeshwa na Mamelodi, alisema Yanga ina timu bora ambapo mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na mwamko wa mashabiki wa timu hiyo.

“Msiwafuate Yanga kwa mazoea watawashangaza itakuwa mechi ngumu kweli, wao (Yanga) wanaona kama walicheza fainali ya Kombe la Shirikisho kwanini sasa wasicheze nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa hiyo watajituma kutafuta ushindi,”alisema Gaye kwenye kipindi hicho.

“Kwanza mnatakiwa kutambua ule Uwanja wa Benjamin Mkapa unachukua mashabiki elfu sitini lakini siku hiyo watakaoingia ni elfu themanini na Yanga ina mashabiki vichaa wanaojua kuipenda timu yao wako tayari kusafiri umbali mrefu kuifuata timu yao.

“Wakati wanaifuata El Merreikh kule Rwanda walisafiri elfu mbili kuifuata timu yao na ikashinda hukohuko kwa hiyo mjiandae msishangae hata mkipoteza kule Tanzania watakuja na huku Afrika Kusini.”

Mamadou aliongeza kwamba Yanga ikiwa chini ya Gamondi, kocha huyo anayeijua vyema Mamelodi ataingia kwenye mchezo kuendeleza msako wake wa kulitwaa taji la Afrika.

HOTELI TATU KUBWA

Kuonyesha kwamba Wasauzi hao wanakuja kwa tahadhari kubwa mpaka jana sio Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala wenyeji wao Yanga ambao walikuwa wanajua kwamba itatua nchini lini na saa ngapi.

Hata hivyo, taarifa za uhakika ni kwamba klabu hiyo inayoendeshwa na bilionea wa madini, Tlhopie Motsepe ambaye ni mtoto wa Patrice Motsepe, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), tayari imeshaweka akiba kwenye hoteli tatu kubwa za hadhi ya nyota tano zilizopo hapa jijini Dar es Salaam.

Chanzo: Mwanaspoti