Wapinzani wa Simba SC katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Power Dynamos wameshinda mchezo wao wa kwanza wa Ligi dhidi ya Nkwazi FC kwa mabao 2-1 kati ya michezo mitatu waliyocheza na kutoka suluhu katika michezo miwili dhidi ya Prison Leopards na Konkola Blades.
Katika mchezo huo dhidi ya Nkwazi FC mabao yalifungwa na wachezaji Owen Tambo na Joshua Mutali ambaye kocha wa Simba Robertinho amemtazama kama mchezaji hatari zaidi katika kikosi cha wapinzani wake.
Katika michezo mitatu ya ligi waliyocheza Power dynamos wamefanikiwa kufunga mabao mawili na kuruhusu bao moja huku wapinzani wao Simba katika michezo miwili ya ligi wamefunga mabao sita na kuruhusu mabao mawili tu katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.
Tangu Agosti 20, Simba haijacheza mchezo wowote wa kimashindano licha ya kucheza michezo mitatu ya kirafiki waliyocheza dhidi ya Cosmopolitan, Ngome na Kipanga FC na kufunga mabao 14 kwa ujumla na kuruhusu bao moja tu.
Tangu Agosti 19 Power Dynamo wao wamecheza michezo mitano ya kimashindano Ligi Kuu pamoja na ligi ya Mabingwa Afrika ambapo wameweza kufunga mabao manne kwa ujumla na kuruhusu mabao matatu.
Katika msimamo wa ligi kwa timu zote Simba amecheza michezo miwili anashika nafasi ya tatu akiwa na pointi 6 sawa na anayeshika nafasi ya kwanza Yanga wakitofautiana idadi ya mabao 6 huku Power Dynamos yeye akishika nafasi ya 6 akiwa na pointi 5 tofauti ya pointi moja na anayeshika nafasi ya kwanza katika ligi yao Nkwazi FC mwenye point 6.
Vigogo Hawa watacheza mchezo wao wa hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika Septemba 16 saa 10 jioni huku Simba akianzia ugenini katika uwanja wa Levy Mwanawasa Zambia.