Kocha wa Chelsea, Graham Potter amekiri mambo bado magumu baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Manchester City, kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliyochezwa uwanja wa Stamford Bridge.
Lakini Potter licha ya kichapo hicho walichapata kwa mara nyingine didi ya Man City, alisifia kiwango bora walichoonyesha kwenye mchezo huo.
Chelsea imeshuka hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoa sare tatu katika michezo nane waliyocheza, huku Potter akiwa na presha kubwa kuhusu mwenendo wake ndani ya klabu hiyo tangu alipotua akitokea Brighton.
Akizungumza baada ya mtanange huo usiku wa kuamkia jana Potter alisema bado kiwango cha Chelsea haijaridhisha hususan kwenye pointi ambazo wamekusanya mpaka sasa.
"Hapana hali hairidhishi kabisa, ngumu sana kuzungumzia hilo, ukiangalia pointi zetu na idadi ya mech tulizocheza utaona, tumecheza mechi tatu za mwisho na matokeo yalikuwa sare, tukapoteza mchezo dhidi ya Arsenal, tukazingua tena dhidi ya Brighton, nadhani ishu kubwa ni jinsi ya kuimarika zaidi," alisema Potter.
Alipoulizwa Potter kama Chelsea ina malengo ya kutinga top four kwenye msimamo wa ligi kocha huyo akajibu kwamba watakuwa na wakati mgumu ndani ya miezi mitano kwasababu raundi ya kwanza ya msimu huu wameshazingua.
"Sitaki kufikiria kitachotokea siku za usoni, tunachotakiwa ni kupambana katika mechi zetu zinazofuata, tuonyeshe kiwango bora kama tulivyoonyesha dhidi ya Man City, ushindani bado unakuja na tutajaribu kuungana kama timu na kuyakabili pamoja," aliongeza Potter.
Chelsea imeendelea kupitia kipindi kigumu baada ya klabu ya Benfica kuwek wazi hawana mpango wa kumuuza Enzo Fernandez anayeuzwa kwa kitita cha Pauni 105 milioni.
Mpaka sasa dili la nyota huyo wa kimataifa Argentina limekufa na hakutakuwa na mazungumzo kati ya Chelsea na Benfica kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na mkali wa masuala ya usajili Fabrizio Romano.
Vile vile Chelsea inakabiliwa na wachezaji wengi majeruhi kama Raheem Sterling, Christian Pulisic, ambao waliumia kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Man City, usiku wa kuamkia jana. Pierre-Emerick Aubameyang alichukua nafasi ya Sterling baada ya kushindwa kuendelea na mchezo huo kipindi cha kwanza.