Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yatupwa 'Jela' ikifa Sokoine

Jela Picture Polisi yatupwa 'Jela' ikifa Sokoine

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Jahazi la Maafande, Polisi Tanzania limeendelea kuzama baada ya leo kukumbana na kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya ndugu zao, Tanzania Prisons na kurudi mkiani.

Kabla ya matokeo ya leo Jumanne, Polisi Tanzania walikuwa wametoka kupata ushindi wao wa kwanza walipoisimamisha Namungo kwa kipigo cha bao 1-0 na kijinasua kwa muda mkiani na sasa mambo yanarudi kuwa mazito kwao.

Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa, Tanzania Prisons walionekana kuwa bora kipindi cha kwanza wakipeleka mashambulizi mengi langoni mwa Polisi Tanzania na dakika ya tatu kupata bao kupitia kwa Jeremiah Juma kwa penalti baada ya beki wa Maafande hao, Omary Chibada kuunawa eneo la hatari.

Bao hilo linakuwa la tatu kwa Straika huyo akiachwa mabao mawili na kinara, Reliant Lusajo wa Namungo na moja dhidi ya Matheo Anthony (KMC) Fiston Mayele (Yanga) na Sixtus Sabilo wa Mbeya City.

Polisi Tanzania walijaribu kupambana kushambulia kupitia kwa nyota wake Idd Kipagwile na Vitalis Mayanga lakini ngome ya Wajelajela ilikuwa imara kudhibiti mipira yote.

Dakika ya 45, Straika Samson Mbangula aliipatia bao la pili na la kwanza kwake msimu huu baada ya kuwachambua mabeki wa upinzani na kumkadilia Kipa, Christopher John na kuukwamishapira wavuni na kuifanya Prisons kwenda mapumziko kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili dakika ya 55 Prisons ilimtoa Joshua Nyantin na kuingia Marco Mhilu, huku Polisi wakiwatoa Salum Kipemba na Rajabu Athuman na kuingia Hamis Kanduru na Abdul Karimu.

Mabadiliko hayo ni kama yaliipa nguvu Polisi Tanzania kutokana na mashambulizi waliyoyafanya lakini Kipa wa Prisons, Edward Mwakyusa alikuwa shujaa kupangua michomo yote.

Dakika ya 75 Prisons iliwapumzisha Dotto Shaban, Hamis Mcha na Samson Mbangula kuwapisha Benjamin Asukile, Michael Ismail na Zabona Hamis na kubadilisha mchezo kwa kuwapa upinzani Maafande kwa mashambulizi ya mara kwa mara japokuwa hayakuwa na madhara wala faida yoyote.

Matokeo hayo yanaifanya Polisi Tanzania kurudi mkiani kwa pointi zao tano sawa na Dodoma Jiji na Ihefu, huku Wajelajela wakipanda hadi nafasi ya tano kwa alama 12 baada ya mechi nane kwa timu hizo.

Chanzo: Mwanaspoti