Timu ya Polisi Tanzania FC imetumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika mjini Moshi baada ya kuichapa Biashara United Mara mabao 2-0.
Mchezo huo wa ligi kuu Bara ulianza kwa kasi katika dakika 45 za kwanza huku Polisi Tanzania wakilishambulia lango la Biashara na kupata bao la kwanza dakika 32 kupitia Deudedity Cosmas aliyeunganisha vyema krosi ya Tariq Seif.
Dakika ya 44,Tariq Seif aliwanyanyua tena mashabiki wa Polisi Tanzania baada ya kupachika bao la pili kwa kuunganisha krosi ya Deusdedity Cosmas "Okoyo" ambayo ilizima kabisa ndoto za Biashara United kuondoka hata na angalau alama moja.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika Polisi Tanzania ilikuwa inaongoza 2-0,kipindi cha pili Biashara ndio walinyanyuka na kuanza kulisambulia kama nyuki lakini hata hivyo uzembe wa safu ya ushambuliaji wa timu hiyo ilifanya Polisi kubaki salama.
Hata hivyo Polisi Tanzania FC nao walijibu mapigo kwa kufanya mashabulizi ambayo hata hivyo hayakuweza kuwa na maana yoyote na kufanya mchezo huo kukamilika wenyeji wakiondoka uwanjani na alama tatu na mabao mawili.
Polisi Tanzania FC sasa imesogea juu hadi nafasi ya saba kwa alama 33 huku Biashara United wakisalia katika nafasi yao ya 15 kwa alama 24.Timu hizo zimecheza mechi 26 kila mmoja.