KLABU ya Polisi Tanzania imeibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Azam katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi.
Mabao ya Polisi Tanzania yalifungwa na Kassim Shaban dakika ya 23, kwa shuti kali lililopigwa na Vitalis Mayanga na kumshinda golikipa wa Azam Mathias Kigonya.
Azam ilisawazisha bao hilo kwa kichwa safi kutoka kwa kiungo mshambuliaji Idd Nado na kumshinda golikipa Metacha Mnata.
Zikiwa zimesalia dakika tano kabla ya kuelekea mapumziko katika kipindi cha kwanza Polisi iliandika bao la pili na la ushindi kupitia kwa mshambuliaji Adam Adam baada ya kuwatoka mabeki wa Azam waliokuwa wamezubaa katika eneo la hatari.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Azam ikihitaji kusawazisha bao hilo ila umakini kwa mshambuliaji wake Idris Mbombo ulikosekana hasa baada ya kukosa nafasi ya wazi dakika ya 64, kwa kupiga shuti kali lililoelekea nje.
Uwanja ulionekana kikwazo kwa timu zote kutokana na mpira kutotulia miguuni mwa wachezaji kutumia zaidi mipira ya juu kama njia mbadala ya kupata matokeo.
Matokeo haya yanainufaisha zaidi Polisi kwani wamejikusanyia alama sita katika michezo miwili iliyoshuka dimbani baada ya mchezo wa ufunguzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Black Rhino Karatu Mkoani Arusha.
Kwa upande wa Azam imeshindwa kupata ushindi katika michezo miwili ya mwanzo baada ya mchezo wa kwanza kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, na 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.