Ni kama Mbeya Kwanza walipanga kuchukua tahadhari yasiwakute ya Gwambina na Ihefu ambao walipanda daraja la Ligi kuu na kushuka msimu uliofata.
Leo Novemba 1, Klabu ya Mbeya Kwanza waliikaribisha timu ya Polisi Tanzania katika dimba la Sokoine Mbeya, ukiwa na muendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Primia Ligi).
Mchezo huo umeisha kwa sare ya magoli 2-2 ambapo wenyeji iliwapasa kutoka nyuma kipindi cha pili na kusawazisha magoli hayo.
Polisi Tanzania ndio waliokuwa wa kwanza kupata magoli yao mawili ambayo yamefungwa na Tariq Seif 24’ na Vitalis Mayanga 44’.
Kipindi cha pili Mbeya Kwanza walirudi kwa kasi na ndani ya dakika 10 wakafanikiwa kusawazisha magoli yote mawili kupitia kwa C. Ngushi 50’ na Yahaya Mbegu ambae amejifunga dakika ya 53 ya mchezo.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha Malale Hamsini wa Polisi Tanzania amesema;
“Kwanza niwasifu wapinzani wetu kwa kupambana na kufanikiwa kurudisha magoli yote mawili ndani ya dakika 10, hakika sio kitu kidogo, wametusoma udhaifu wetu na wameutumia kutuadhibu”.
Kwa matokeo hayo Polisi Tanzania imepanda mpaka nafasi ya pili ikiwa na alama 10 baada ya kucheza michezo mitano huku Mbeya kwanza wakibaki nafasi yao ya sita wakiwa na alama saba.