Wakati homa ya mchezo wa Ligi Kuu NBC kati ya Polisi Tanzania FC na Yanga SC utakaopigwa kesho Jumapili ikizidi kupamba moto kiingilio cha chini katika mchezo huo imetajwa kuwa ni Sh 5000.
Mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na ubora wa vikosi vyote utapigwa katika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa ambapo Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Hassan Juma amesema wamepanga kuweka kiingilio cha chini kuwa Sh5,000 ili kutoa fursa kwa wapenzi wa soka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga kujitokeza kwa wingi siku hiyo.
"Kama kawaida kingilio sisi tumeweka kuwa ni Sh5000 mzunguko, 10,000 VIP A na B, VVIP ni 20,000 lengo letu ni kutoa fursa kwa mashabiki wa soka mkoani hapa na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kuja kushuudia Yanga anavyokufa" amesema Juma.
Ameongeza kuwa tiketi hizo zinapatikana katika katika ofisi za TTCL Arusha ,Jinsi gulio mkabala na Golden Rose , uwanja wa Sheikh Amri Abeid pamoja na Keto Pharmacy Sanawari huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi mapema hili kuepuka usumbufu kesho.
Alisema Yanga ni timu kubwa wazoefu katika ligi, timu yenye wachezaji wazuri wengi na wenye uzoefu na ligi kwa hiyo wao hawaidharau kabisa lakini waje wakiwa wamejipanga wakijua wana kuja kupambana na Polisi Tanzania ambao rekodi katika uwanja wake wa nyumbani inambeba ivyo mchezo hautokuwa mwepesi kwa Yanga kama wavyodhani.
Amesema tayari mwalimu wa timu Malale Hamsini amefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo na amewahakikishia wana Kilimanjaro, Arusha na Manyara kubakisha alama tatu ambayo itakuwa ni zawadi hasa baada ya kucheza mechi nne mfululizo bila ushindi.
“Sendoff walishafanya ndugu zetu Mbuni sisi kesho tunakuja kumchukua mwali wetu niwahakikishie kwamba Yanga kesho anakufa wala msiwe na wasiwasi” amesema Juma
Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amewataka mashabiki wao kujitokeza mapema kukata tiketi kwa N-Card hili kuwapa uwepesi wa kuingia mapema bila shida huku akiahidi kuwafurahisha kama walivyofanya kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union kule jijini Tanga.