Shoo za Ligi Kuu Bara zinaendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakakutanisha maafande wa Polisi Tanzania itakayoialika Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi huku timu zote zikitambiana kwamba dakika 90 hazitakuwa za kitoto kwani kila moja inataka pointi tatu.
Timu hizo zinakutana kila moja ikiwa kwenye nafasi isiyoridhishwa nayo katika msimamo, hali ikiwa mbaya zaidi kwa Polisi inayonolewa kwa sasa na Kocha Mwinyi Zahera.
Polisi ipo nafasi ya pili toka mkiani ikiwa na pointi 15, wakati Kagera iliyopo chini ya Mecky Maxime inakamata nafasi ya tisa na pointi zao 25 na matokeo yoyote kwa timu mojawapo itawabeba kiaina kwenye msimamo huo wa timu 16 unaongozwa na Yanga yenye alama 59.
Kocha msaidizi wa Polisi, John Tamba alisema maandalizi kwa upande wao yamekamilika vijana wake wako katika morali na ari kubwa kushinda na kupambana kukwepa kushuka daraja.
Alisema Kagera ni timu nzuri ina wachezaji wazuri lakini kama Polisi walishajiwekea mikakati ya kuhakikisha mechi zote zilizosalia wanashinda na kubaki kwenye Ligi ambayo ndio malengo yao makubwa huku wakiziombea vibaya timu zilizopo juu yao.
“Tunaenda kukutana na timu nzuri lakini tumejipanga kuwakabili na kubakisha alama Tatu nyumbani kwa sasa hatuhitaji kupoteza hata mchezo mmoja kutokana na nafasi mbaya tuliyopo” alisema Tamba, huku Maxime alisema wanatambua wanaenda kukutana na timu ya namna gani hivyo ameandaa kikosi kwenda kupambana nao na kushinda ambayo ndio nia yao.
“Haitakuwa mechi rahisi kwa nafasi iliyopo Polisi, lakini tunachokitaka ni kupata alama tatu zitusaidia kusogea eneo zuri la msimamo,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars.