Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pogba yupo gizani

PAUL POGBA Pogba yupo gizani

Mon, 27 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Swali kwa mashabiki wa soka kuhusu safari ya Paul Pogba ndiyo imemalizika au tuendelee kusubiri?

Mashabiki wa soka kwa sasa wengi wanajiuliza kuhusiana na kiungo huyo kama ataendelea kukiwasha kwa kiwango cha juu.

Hii ni kutokana na kile ambacho kinamkumba kiungo huyo ambaye kwa sasa muda wake mwingi yupo bize kuuguza majeraha.

Hakuna asiyejua ubora wa Pogba na kazi ambayo amekuwa akiifanya uwanjani. Mashabiki wa soka kiukweli wameumisi moto wa kiungo huyo.

Mashabiki wa Juventus na Ufaransa ndiyo wanaonekana kummisi zaidi nyota huyo ambaye ni mchezaji wao anayetarajiwa kukaa nje kuuguza majeraha kwa mwezi baada ya kuumia.

Ufaransa walianza kummisi Pogba katika Kombe la Dunia 2022 pale timu yake ikifika fainali, yeye alikuwa jukwaani akiuguza majeraha.

Lakini hapohapo Juventus walikuwa wana hamu ya kuona kiungo wao huyo anarejea uwanjani na kuibeba timu yao ambayo imekuwa ikipita katika wakati mgumu.

Kumbuka kuwa mwisho wa msimu uliopita Pogba aliondoka Manchester United ambako alikuwa hapo tangu mwaka 2016, hakucheza kwa mafanikio makubwa kama wengi walivyotarajia kutokana dili lake la uhamisho kuwa la bei mbaya, zaidi alifanikiwa kutwa taji la Europa League pekee akiwa hapo mwaka 2017.

Msimu wa 2022-23, Pogba alitua tena Juventus lakini tangu ametua hapo amekuwa nje ya uwanjani zaidi ya siku 200, hivi karibuni alirejea uwanja wakati Juventus wakicheza dhidi ya Torino.

Hii ilikuwa ni mechi yake ya kwanza ya mashindano tangu ajiunge na Juventus. Lakini wakati mashabiki wakiwa na furaha kuwa kiungo wao amerudi, mambo yakabadilika tena.

Mechi iliyofuata Pogba akafanya makosa ya kinidhamu na kocha Massimiliano Allegri akamuweka kando kiungo huyo.

Wakati akitumikia adhabu, akiwa mazoezini Pogba akaumia, majibu yalipotoka ni kwamba kiungo huyo atakuwa nje tena kwa mwezi na hii ndiyo unaona namna gani Juventus ambavyo wanaumia kumpoteza kiungo huyo ambaye hakuna asiyejua ubora wake.

Hapa ndio unajiuliza Pogba ambaye hivi karibuni ametimiza miaka 30 atarudi katika ubora wake kama zamani? Ataweza kuwafurahisha mashabiki wa Juventus tena au ndiyo habari yake imeishia hapo? Tusubiri.

Kumbuka kuwa Juventus wanamuhusudu sana kiungo huyo kwani huko nyuma aliwahi kutisha akiwa hapo.

Kabla ya msimu huu, huko nyuma Pogba alicheza mechi 179 akifunga mabao 34 na asisti 40.

Akiwa hapo, alitwaa mataji manne ya Serie A, Coppa Italia (2), Supercoppa (2). Aliwahi kuwa mchezaji bora wa Serie A mara moja na wa Juventus mara moja, hizo zilikuwa ni nyakati bora kabisa kwa Pogba enzi zake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live