Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pogba alivyojiingiza kwenye msala wa dawa haramu

Pogba  490 1140x640.png Paul Pogba

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Supastaa, Paul Pogba yupo kwenye hatari ya kukumbana na adhabu ya kufungiwa kucheza soka kwa miaka miwili baada ya kufeli kwenye vipimo vya matumizi ya dawa zinazopigwa marufuku michezoni.

Kiungo huyo wa Juventus, ambaye kwa sasa ametumikia adhabu ya muda akisubiri uchunguzi wa kina na hukumu yake kutolewa, amewekwa kwenye wakati mgumu na mamlaka zinazopinga matumizi ya dawa haramu huko Italia.

Pogba alifanyiwa vipimo baada ya mechi ya Juventus ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Udinese iliyofanyika Agosti 20, mwaka huu.

Hofu kubwa ilitanda awali kwamba huenda staa huyo akafungiwa hadi miaka minne, lakini hii ripoti mpya ya kusema kwamba anaweza kufungiwa miaka miwili, itamfanya Pogba arejee uwanjani akiwa na umri wa miaka 32.

Hata hivyo, staa huyo wa zamani wa Manchester United hatakuwa mchezaji wa kwanza endapo kama atakumbana na adhabu ya kufungiwa kwenye soka kwa matumizi ya dawa zinazokatazwa baada ya kuwapo na mastaa kibao.

Andre Onana

Kipa wa Manchester United, Andre Onana alifungiwa na Shirikisho la soka la Ulaya miezi 12, Februari 2021, baada ya kupimwa na kukutwa ametumia dawa aina ya Furosemide. Kipa huyo Mcameroon alidai kwamba alimeza kimakosa dawa za ujauzito za mke wake. Baada ya kukata rufaa na uchunguzi wa kutosha, adhabu yake ilipunguzwa hadi miezi tisa.

Adrian Mutu

Baada ya kuanza vizuri kabisa msimu wake wa kwanza huko Chelsea iliyokuwa chini ya Kocha Jose Mourinho, staa huyo wa Pauni 15.8 milioni, aliyesajiliwa katika kipindi cha majira ya baridi, Mutu, alijikuta akifungiwa soka kwa miezi saba baada ya kupimwa na kukuta ametumia cocaine mwaka 2004. Mutu akajiharibia sifa yake huko Stamford Bridge na kujikuta akiwekwa kando licha ya kudhaniwa kwamba angekuwa kitu kikubwa sana kwenye Ligi Kuu England.

Diego Maradona

Mchezaji maarufu zaidi kuwahi kuingia kwenye kashfa ya kufungiwa kutokana na matumizi ya dawa zijazopigwa michezo alikuwa staa wa zamani wa Argentina, Diego Maradona. Mkali huyo wa zamani wa Napoli alipimwa na kukutwa ametumia cocaine mwaka 1991. Maradona alifungiwa miezi 15 na kupigwa faini ya Dola 70,000. Kombe la Dunia 1994, Maradona alipimwa na kukutwa ametumia dawa aina ya ephedrine. Akaondoshwa kwenye mashindano.

Mark Bosnich

Kipa wa zamani wa Chelsea, Mark Bosnick naye aliwahi kukutwa na tatizo la kufeli vipimo vya matumizi ya dawa zinazokatazwa michezoni. Bosnich alipimwa na kukutwa ametumia cocaine, Septemba 2002 na alifungiwa kucheza soka kwa miezi tisa. Baadate, Bosnich alikiri kutumia cocaine, lakini akidai alitumia kipindi ambacho ameshaachana na soka. Vinywaji alivyokuwa akinywa Bosnick kwenye kumbi za starehe za usiku ndivyo vilivyodaiwa kuwa na viungo vinavyopigwa marufuku michezoni.

Kolo Toure

Kolo Toure, staa wa zamani wa Arsenal na Manchester City alipimwa na kukutwa ametumia dawa zinazokatazwa michezoni na hivyo kujikuta akikumbana na adhabu mwaka 2009. Kolo alifungiwa miezi sita. Beki huyo wa zamani wa Ivory Coast, alidai alikuwa anatumia vidonge vya mkewe vya kupunguza uzito. FA ililichukulia jambo hilo lisilokua la makusudi.

Samir Nasri

Staa mwingine wa zamani wa Arsenal na Manchester City, Samir Nasri naye alikumbana na adhabu mwaka 2018 kwa kosa alilofanya mwaka 2016. Mfaransa huyo alifungiwa miezi sita baada ya kujitibu kwa njia isiyosahihi kwa wanamichezo katika kliniki moja huko Los Angeles, Marekani. Nasri alikwenda kuwekewa dripu maalumu ya maji ili kumfanya asipungukiwe maji kwa muda wote atakaokuwa uwanjani. Wakati huo Samir alikuwa akiichezea Sevilla ya Hispania kwa mkopo akitokea Man City.

Pep Guardiola

Wakati sasa akitambulika kama mmoja wa makocha matata kabisa kwenye soka, Pep Guardiola, mwaka 2001, alikumbana na adhabu ya kufungiwa miezi minne baada ya kutumia dawa zinazokatazwa michezoni. Kipindi hicho alikuwa akiichezea Brescia ya Italia, ambapo alikutwa na hatua ya kutumia dawa aina ya Nandrolone. Baadaye alikata rufaa na adhabu ikaondoshwa.

Chanzo: Mwanaspoti