Kocha Mauricio Pochettino, amelalamikia ugumu wa Chelsea mbele ya lango baada ya kutoka suluhu na Bournemouth juzi Jumapili (Septemba 17).
Katika mchezo wa pili mfululizo “The Blues’ hao walishindwa kupata bao licha ya kuwa na mashuti 14 yaliyolenga lango na wamefanikiwa kufunga mabao matano pekee katika mechi tano za Ligi Kuu msimu huu.
Akizungumza na tovuti rasmi ya klabu baada ya sare hiyo, Pochettino alibainisha matatizo ya Chelsea mbele ya lango kuwa ndio msingi wa kushindwa kwao kushinda michezo.
“Nafikiri tena tunatakiwa kukamilisha nafasi ambazo tunatengeneza. Katika dakika 20 au 25 za kwanza tulistahili kufunga, lakini hatukupata bao.
“Mwishowe mchezo ulikuwa wazi, katika dakika 15 au 20 za mwisho, nadhani tulitaka kushinda, wakati mwingine tulianza kuharibu safu yetu kwa sababu beki wa pembeni alikuwa juu sana, jambo ambalo liliipa Bournemouth uwezekano wa kufanya mashambulizi mengine.
“Tunahitaji kustarehe zaidi. Wakati mwingine wachezaji wa ulinzi wanataka kusaidia kwa sababu hisia ni kwamba tunatengeneza nafasi, lakini hatufungi, basi tunahitaji kuwa wajanja lakini wachezaji wengi bado wanajifunza kuhusu mchezo. Hiyo hutokea wakati tunaunda timu mpya yenye maeneo mengi tunayohitaji kuboresha.