Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans van der Pluijm, amefunguka kuwa, bado anaendelea kuwaandaa wachezaji wake kwa ajili ya mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Mbeya City.
Mchezo huo wa hatua ya robo fainali, unatarajiwa kupigwa kesho Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Liti uliopo mkoani Singida.
Akizungumza nasi, Pluijm alifunguka: “Maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Mbeya City bado yanaendelea, programu yetu ya mazoezi tuliyofanyia mkoani Dodoma imefanikiwa kwa asilimia zote.
“Wachezaji wapo fiti japokuwa niliona mapungufu machache kwenye mechi yetu ya kirafiki dhidi ya Dodoma Jiji ambayo tulipata ushindi wa mabao 1-2 na tayari tunafanyia maboresho ili yasiweze kujitokeza kwa Mbeya City.
“Dodoma Jiji ni kipimo kikubwa kwetu kwa sababu ni timu nzuri yenye morali ya ushindani, ukizingatia Mbeya City ni wapinzani wakubwa hasa kwenye mechi hizi za mtoano, hivyo naamini tutafanikiwa kupata ushindi mbele yao kwa sababu tulijipanga vya kutosha.”