Licha ya Singida Big Stars kushinda mabao 3-0 dhidi ya Polisi Tanzania ila kocha wa timu hiyo, Hans Van Der Pluijm amewataka wachezaji wa kikosi hicho kuongeza umakini zaidi kutokana na kupoteza mipira bila sababu.
Akizungumza nasi, Pluijm alisema licha ya ushindi ila hakufurahishwa na kitendo cha wachezaji wa timu hiyo kupoteza mipira kizembe kwani laiti wangecheza na washindani wazuri ingeweza kuwaletea matatizo.
"Ushindi ni mzuri kwetu kwa sababu tunaendelea kushikilia nafasi yetu ya tatu ingawa baada ya mchezo nilikaa na wachezaji wote na kuwahisi kuongeza umakini wakati tukiwa na mpira kwani ni njia salama ya kujilinda."
Aidha Pluijm aliongeza siri kubwa ya kufanya vizuri hadi sasa ni kutokana na ushindani wa namba uliopo kwa wachezaji wenyewe.
"Kila nafasi inapokuwa na wachezaji zaidi ya wawili wazuri basi ushindani utaongezeka kwa sababu kila mmoja wao atataka kucheza na ili apate namba ni lazima atajituma mara mbili zaidi jambo ambalo ni manufaa kwetu."
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida, mabao ya Singida BS yalifungwa na Pascal Wawa na Nickson Kibabage ambao ni ya kwanza kwao na kikosi hicho huku la tatu likifungwa na Amissi Tambwe.