Simba ijipange dhidi ya Singida Big Stars katika mchezo wao wa leo Ijumaa, kwani kocha Hans Pluijm ameandaa mbinu za kuifunga,Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mechi ya raundi ya kwanza iliyopigwa Novemba 9, Uwanja wa Liti uliopo Singida, timu hizo zilitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1, yafungaji Deus Kaseke (SBS) na Peter Banda (Simba).
Katika mazoezi yao ya juzi, waliyoyafanya Uwanja wa Uhuru, kocha Pluijm alikuwa anawaelekeza zaidi washambuliaji wake kufunga mashuti ya umbali mrefu, na kutumia mbinu ya kupita pembeni akitumia mawinga kupandisha mashambulizi.
Alipoulizwa kuhusiana na mechi dhidi ya Simba, alikiri hautakuwa mchezo mwepesi lakini pointi tatu kwake ni muhimu na anakiamini kikosi chake na tayari amekipa mbinu.
Alisema anawaheshimu Simba na anafahamu ni timu ambayo inacheza mpira wa chini kwa kupigiana pasi fupi fupi huku ikitumia zaidi viungo kuibeba timu na ndio maana amejaribu kutafuta njia mbadala kwa kuandaa mawinga ikitokea eneo la kiungo wakadhibitiwa.
"Nimekiandaa kikosi changu kulingana na aina ya uchezaji wa Simba, utakuwa mchezo wa kimbinu zaidi na ufundi, kikubwa tumejipanga na tupo tayari kwa kazi" alisema.
Pluijm alisema anatarajia mchezo Bora na wa ushindani huku kila timu ikisaka pointi tatu muhimu kwaajili ya kumaliza mzunguko wa pili ambao amekiri kuwa ni wa mapambano kila mmoja anataka kumaliza vizuri.
Kwa upande wa beki wa zamani wa Simba, Pascal Wawa ambaye kwa sasa yupo SBS alisema anaamini utakuwa mchezo mgumu ila timu yake itashinda mechi.
"Naiheshimu Simba ila kwa upande wa kazi nikiwa uwanjani dakika 90 akili na nguvu zangu zinakuwa kuitetea timu yangu kupata pointi tatu, ndio maana nasisitiza utakuwa mchezo wa kuvutiwa.
"Japo SBS ni ngeni kwenye Ligi Kuu,lakini tunataka kuionyesha Simba sisi ni washindani na tunahitaji nafasi za juu na timu yetu tupo wachezaji wazoefu, ambao tutataka kulinda heshima yetu."
Kagere v Ajibu
Kuna wakati mastaa wanakuwa na utani wao, ndicho kilichotokea baina ya straika Meddie Kagere na Ibrahim Ajibu ambaye alicheza naye Simba. Katika mazoezi yao ya jana, Kagere muda mwingi alionekana kumtania Ajibu,huku akimwagia maji ambayo waliwekewa kwa ajili ya kunywa.
Ajibu alionekana muda mwingi anatabasamu kila alipokuwa karibu na Kagere na kujikuta wawili hao wanajikuta wapo pamoja muda mwingi na wote wanacheza nafasi za mbele.