Baada ya kutolipwa mshahara kwa kipindi cha miezi minne, kocha Pitso Mosimane amevunja mkataba na Al Ahli Saudi FC ya Saudi Arabia na sasa anapatikana katika soko la usajili.
Taarifa za kuondoka kwa Pitso ndani ya Ahli zimethibitishwa na Moira Tlhagale.
“Ndiyo, Kocha Pitso amejiuzulu Al Ahli. Tumepokea simu nyingi kutoka Mashariki ya Kati na Uarabuni. Bado tupo kwenye mapumziko na tutarejea Afrika Kusini, Ijumaa (kesho). Tutaendelea kuzungumza na timu zinazomhitaji Pitso na pale tutakapota timu sahihi basi atakwenda,” amesema Tlhagale akizungumza na Sunday World jana Wednesday.
“Hatuna uhakika kama Pitso atarudi kufundisha Soka la Afrika Kusini (Ligi Kuu ya PSL), hatuwezi kusema ndiyo au hapana, hatuwezi kusema chochote juu ya hilo," alisema.
Siku za hivi karibuni, Pitso amekuwa akihusishwa kwenda nchini Atunisia kufundisha miamba ya soka nchini humo, Esperance, Super Eagles ya Nigeria huku pia Kaizer Chiefs nao wakitajwa kumuwinda.
Aidha, Tlhagale alisema hawajazungumza na Timu yoyote ya Taifa lolote licha ya tetesi kusema kuwa zipo baadhi ya timu za Taifa ambazo zimekuwa zikitaka huduma yake ikiwemo Bafana Bafana ya Afrika Kusini.
“Ninasiki tetesi kuwa kuna timu za taifa Barani Afrika zinamtaka Pitso na zimewasiliana naye, lakini hatujapata taarifa zozote rasmi kutoka timu yoyote ya Taifa," amesema Tlhagale.
Mosimane na benchi lake la ufundi wakiwemo Kabelo Rangoaga, Musi Matlaba, Kyle Solomon na Maahier Davids wameingia kwenye mgogoro na Ahli baada ya kutolipwa mishahara yao na marupurupu mengine kwa miezi kadhaa jambo ambalo limewafanya kwenda FIFA kupeleka malalamiko yao.
Keshokutwa, Jumamosi, Mosimane atazindua shule yake ya kukuza vipaji vya sokahuko Sandton, Johannesburg.
Kufuatia kocha Nasreddine Nabi kuondoka Yanga, Je, ni wakati wa klabu hiyo kumuwinda Mosimane kurithi mikoba ya Nabi?