Kocha wa zamani wa Mamelodi Sundowns, Al Ahly ambaye kwa sasa anafundisha klabu ya Al-Wehda ya United Arab Emirates, Pitso Mosimane raia wa Afrika Kusini, amesema sio kwamba makocha wa Afrika hawana vigezo vya kufundisha timu za Ulaya, bali timu za Ulaya ndio hazitaki kukubali kuajiri makocha wa Afrika.
“Mpira hauhusu wapi unatokea. Tunaweza kuzunguka na kuleta visingizio lakini ni rahisi tu, Ulaya haitaki kuajiri Makocha wa Kiafrika.
“Kazi yangu ni kujenga imani na kumbukumbu ya kudumu kwa Makocha wa Kiafrika na kuwafanya waseme ‘Angalia,Ninafikiria kuna kitu Afrika’, tuwape nafasi.
"Ulaya bado haikubali kocha wa Kiafrika. Wanakuja kununua wachezaji kuwasaidia washinde Klabu Bingwa Ulaya. Sadio Mane na Mohamed Salah walikuja kuwasaidia Liverpool kushinda Klabu Bingwa kama Neymar na Messi.
“Kama ukiangalia usajili,kiasi gani walilipa kuwasajili Sadio Mane na Mo Salah na kiasi gani walilipa kwa wachezaji wa Amerika Kusini.?”
“Wanatakiwa kubadili mitazamo yao kwa Waafrika. Kylian Mbappe ana asili ya Afrika. Sawa na N’Golo Kante na Karim Benzema. Ulaya inalishwa na Afrika.
“Nilikuwa naangalia klabu bingwa Ulaya, nikaona wachezaji Waafrika wote wanacheza. Sasa wako wapi makocha wa Afrika?Wana wachezaji wa Afrika tu.
"Unaweza kusema makocha wa Afrika wanatakiwa wawe na ubora fulani, ni sawa, Mimi nipo hapa,” amesema Pitso Mosimane kupitia AD Sports.
Akiwa na Makombe matatu ya Klabu Bingwa Afrika, hakuna kocha wa Afrika aliyeshinda idadi hiyo ya makombe kama Pitso.
“Makocha wangapi wa Ulaya wameshinda Klabu Bingwa Ulaya mara 3? Si wengi. Carlo Ancelotti mara 4 ,Pep Guardiola pengine mara tatu, Jurgen Klopp mara moja, kwa hiyo ni vigumu” aliongeza.
“Kama ukishinda klabu bingwa Afrika, haimanishi pia ninaweza kushinda Asia au Ulaya? Unadhani klabu kama Bayern Munich itakuja kwangu?!
“Kiuhalisia. hawatakuja ila tuache kusema kuhusu Bayern. Tuongee kuhusu Red Bull Salzburg,Leipzig au West Ham. Unadhani wana kocha ambaye ameshinda makombe kama mimi? hakuna hata mmoja.”