Kocha wa zamani wa Al Ahly Pitso Mosimane ameiongoza klabu yake ya Al Ahli Saudi kutwaa ubingwa wa Ligi daraja la kwanza Nchini Saudi Arabia kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Al-Qadisiyah FC.
Ushindi huo umeifanya Al Ahli kufikisha pointi 71 kwenye msimamo wa ligi na kujihakikishia ubingwa baada ya wapinzani wake karibu Al Akhdood (alama 65) kupokea kichapo cha 3-2 dhidi ya Al Sahel SC na kuporomoka mpaka nafasi ya tatu huku Al Hazem FC (alama 67) ikikwea mpaka nafasi ya pili.
Mosimane aliichukua Al Ahli ikiwa nafasi ya tano na kuiongoza kushinda mechi 18, sare 6 na vipigo vitatu na kuipandisha daraja kwenda Ligi kuu ya Saudi Pro sambamba na kutwaa ubingwa huo wa kihistoria.
Mosimane ametwaa kombe lake la 19 katika maisha yake ya ukocha likiwa ni kombe lake la kwanza akiwa nje ya Afrika.
Akiwa SuperSport United ya Afrika Kusini, Mosimane akishinda kombe ka SAA Super Eight na kombe la Nedbank.
Mosimane alipata mafanikio makubwa akiwa Mamelodi Sundowns baada ya kushinda makombe 5 ya Ligi kuu, makombe 2 ya Nedbank, makombe 2 ya Telkom Knockouts, Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja na CAF Super Cup mara moja.
Akiwa na klabu ya Al Ahly ya Misri, Mosimane alishinda Ligi ya Mabingwa Afrika mara 2, CAF Super Cup mara 2 sambamba na kombe la Misri mara moja.
Licha ya mafanikio hayo inaelezwa kuwa klabu Al Ahli Jeddah haipo tayari kumuongeza mkataba mpya huku ikidaiwa ipo sokoni kutafuta kocha mwingine atakayeinoa klabu hiyo kwenye Saudi Pro League.