Mkufunzi Pitso Mosimane raia wa Afrika Kusini amechaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi Februari wa Ligi daraja la kwanza Nchini Saudi Arabia baada ya kuwa na mwenendo mzuri ndani ya klabu ya Al Ahli Jeddah Saudi inayosaka tiketi ya kurejea Ligi kuu ya Saudi Pro msimu ujao.
Mosimane ameiongoza klabu hiyo kushinda mechi 13, sare 5 na vipigo viwili tangu achukue mikoba ya kuinoa mnamo Septemba mwaka Jana akiitoa kutoka nafasi ya 7 mpaka nafasi ya pili alama moja nyuma ya kinara Al Hazem FC.
Al Ahli ambayo pia ipo kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa Ligi hiyo ilishinda mechi tatu na kupoteza mchezo mmoja ndani ya mwezi Februari huku kikosi hicho kikitajwa kama kikosi chenye rekodi bora ya ulinzi kikiwa kimeruhusu magoli 17 tu kwenye mechi 25 mpaka sasa msimu huu.
Zikiwa zimesalia mechi 9 pazia la Ligi hiyo kufungwa Mosimane anahitaji alama 18 tu ili kujihakikishia nafasi kwenye Ligi kuu ya Saudi Pro League alipo Cristiano Ronaldo na Al Nassr FC.
“Ninapokea tuzo hii kwa unyenyekevu kwa niaba ya wachezaji, wafuasi wetu, mashabiki, Wasimamizi, wafanyakazi, bodi na makamu wa Rais na Rais wa timu na familia zetu. Ni tuzo yetu na sote tulichangia. Pia bila kusahau wafadhili na wote waliotupigia kura. Shukran ” ameandika Pitso Mosimane kwenye ukurasa wake Twitter.