Nchi itasimama!! Ni michezo miwili mikubwa ya wawakilishi wa Tanzania, Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa, watakuwa mzigoni wikiendi hii kwenye Uwanja wa Mkapa kupigania heshima na pointi ambazo zitawaweka pazuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba ipo Kundi C kwenye Ligi ya Mabingwa wataanza kutupa karata yao, Jumamosi dhidi ya Raja Casablanca ambao waliitandika Vipers ya Uganda mabao 5-0 huku Yanga ikiikaribisha TP Mazembe kesho Jumapili.
Hii ni nafasi kwa wawakilishi hao wa Tanzania kuweka hai matumaini ya kuvuka hatua ya makundi kufuatia kuanza michuano hiyo kwa kupoteza michezo yao ya kwanza, Simba alifungwa bao 1-0 dhidi ya Horoya kisha Yanga ikafungwa 2-0 dhidi ya US Monastir, Tunisia.
Wakiwa kwenye opareshi mbili tofauti kwenye michuano hiyo ya kimataifa, wababe hao wa soka la Tanzania wamepewa motisha na Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye ameeleza kuwa kila bao ambalo watafunga kwenye ushindi wao atatoa Sh. 5milioni.
Kulingana na ubora wa wapinzani wa Simba na Yanga, Raja Casablanca na TP Mazembe, hizi ndio bato zinazotarajiwa kuamua matokeo yao.
SIMBA v RAJA CASABLANCA
Yapo maeneo matatu muhimu, ukuta, kiungo na ushambuliaji yote hufanya kazi kwa pamoja na ufanisi wake hutofautiana ni timu chache sana ambazo zimekuwa na ubora unaolingana katika maeneo yote hayo, nyuma ukuta wa zege, kiungo cha moto na safu yake ya mbele ni kiwembe.
Siku chache zilizopita, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Morocco akiwa na Wydad Casablanca, alieleza vile Simba inapaswa kumdhibiti winga hatari wa Raja Casablanca, Zakaria Habti. Licha ya Raja Casablanca inasura chache mpya kutokana na kuondoka kwa Ben Malango na Soufiane Rahimi, Msuva alisema bado staili yao ya uchezaji ni ileile, “Wapo wachezaji ambao nilishindana nao mfano ni huyo, Zakaria ni hatari sana, sio mchezaji wa kumwachia nafasi, nimesikia bado anaendelea kufanya vizuri.”
Kwa mujibu wa Msuva inamaana kuwa ubora wa Raja ni katika maeneo yake ya pembeni, hivyo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe wanapaswa kuwa macho pale ambapo watakuwa wakishambulia, wasijisahau.
Mshambuliaji huyo wa Kitanzania, hakuishia hapo, alisema, mbali na Zakaria wachezaji wao mwingine ambao ameona wanafanya vizuri ni pamoja na Abdelilah Hafidi, Yousri Bouzok, Mohammed Nahiri na Hamza Khabba. “Jambo muhimu kwa Simba ni kucheza kwa tahadhari.”
Wakati kukitarajiwa kuwa na bato kubwa kwenye maeneo ya pembeni ambako Simba napo ni hatari kutokana na kuwa na mawinga wenye spidi kama vile Pape Sakho, shughuli nyingine inaweza kuwa kwenye eneo la kiungo hasa cha juu ambapo wekundu hao wa Msimbazi wamekuwa bora kutokana na uwepo wa Clatous Chama, ikumbukwe kuwa Sadio Ntibazonkiza naye anarejea kikosini.
Licha ya Simba kukosa huduma ya Sadio Kanoute ambaye atakuwa akitumikia adhabu ya kadi za njano mfululizo, bado yapo machaguo ya wachezaji kama vile Mzamiru Yassin, Ismael Sawadogo, Jonas Mkude na Nassoro Kapama ambao wanaweza kutumika kwenye eneo la kiungo cha chini.
Shoo ya Simba dhidi ya Raja inaweza kumalizwa kwenye maeneo hayo lakini pia vijana wa Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wanatakiwa kuwa makini na mipira ya faulo na kona ili kuwa salama kwani wapinzani wao ni wazuri eneo hilo.
YANGA v TP MAZEMBE
Changamoto kubwa ambayo ilikuwa nayo TP Mazembe ni ubutu wa safu ya ushambuliaji, kocha wa kikosi hicho, Mihayo Kazembe ameinoa na matunda yake yalionekana kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Real Bamako.
Mazembe imekuwa na michezo mingi ya kirafiki ili kuwa kwenye kiwango bora cha ushindani kwani ligi yao ya ndani ilimalizika mwishoni mwa mwaka jana, hivyo mabeki wa Yanga wakiongozwa na Yannick Bangala na Dickson Job wanapaswa kuwa na macho na Alex Ngonga kwani ni mmoja wa washambuliaji hatari wa timu hiyo.
Licha ya Yanga kupoteza mchezo wake wa kwanza ilimiliki wa mchezo, hivyo ni wazi inaweza kuendeleza hilo lakini inatakiwa kuongeza umakini kwenye safu yao ya ushambuliaji.
Bila shaka Mihayo ataandaa mapango wa kumdhibiti, Fiston Mayele kwani taarifa zake ni kubwa na wajau vile ambavyo amekuwa moto wa kuotea mbali akiwa na kikosi cha Wananchi hivyo kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi naye anapaswa kuwa na mbinu mbadala ili kufanya vizuri.
Yanga itakuwa na kazi kwenye eneo la kujilinda lakini pia Mazembe itakuwa na kazi kutokana na ubora wa timu zote mbili kwenye maeneo hayo, Nabi anajivunia ubora wa kiungo Azizi Ki anayeweza kuwa ufunguo wa mashambulizi.
Akiongea Mihayo alinukuliwa akisema,”Yanga ina wachezaji wazuri hasa eneo la ushambuliaji wana Fiston (Mayele) ni mchezaji aliye katika kiwango bora lakini pia wana mchezaji ametokea Zambia wamemsajili hivi karibuni (Musonda) tunatakiwa kuwa na ubora wa kuwadhibiti.