Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pira litapigwa kwa Mkapa

Yanga Kikosi Vs Ruvu Yanga wakipasha

Sat, 4 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni hesabu za kibingwa tu ambazo Yanga inazipiga kwa sasa ikianzia leo wakati itakapokuwa nyumbani kuikaribisha Namungo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 12.30 jioni.

Katika mechi tisa ilizobakiza, Yanga ikishinda saba zinazofuata itakuwa imejihakikishia rasmi taji la Ligi Kuu msimu huu na kati ya mechi hizo saba, mojawapo ni dhidi ya Namungo.

Ushindi dhidi ya Namungo sio tu utaifanya Yanga ifikishe jumla ya pointi 59 ambazo zitaiwezesha kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi, lakini kuzidi kutengeneza presha na ugumu kwa washindani wake kwenye mbio za ubingwa hasa Simba iliyo katika nafasi ya pili.

Kwa Namungo iliyo nafasi ya sita, ushindi dhidi ya Yanga leo utaisogeza hadi katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi kwani itafikisha jumla ya pointi 32 na kuweka hai matumaini ya kumaliza katika nafasi nne za juu.

Ni mlima mrefu zaidi kwa Namungo hasa ukizingatia inakutana na safu kali ya ushambuliaji ya Yanga, huku yenyewe ikiwa na ukuta mwepesi kwani katika mechi 21 ilizocheza, timu hiyo imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 21 ikiwa ni wastani wa bao moja kwa kila mechi wakati Yanga imefunga mabao 39 ikiwa ni wastani wa bao 1.9.

Mechi za ligi baina ya Namungo na Yanga huwa na ushindani wa hali ya juu na kuthibitisha hilo, timu hizo zimewahi kukutana mara saba ambapo Yanga imepata ushindi mara moja na mechi nyingine sita zilizobakia zilimalizika kwa sare. Mechi hiyo ni ya duru la kwanza Yanga ikishinda 2-0 mjini Lindi.

Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amekiri ushindani ambao wamekuwa wakiupata dhidi ya Namungo ingawa ametamba kuwa wamefanya maandalizi mazuri kuhakikisha wanapata ushindi huku akisema wachezaji watakaokosekana ni wawili tu ambao ni majeruhi.

"Namungo ni timu inayopenda kucheza kwa nguvu sana na matokeo yao yaliyopita dhidi ya KMC yanawapa confidence ( kujiamini ) lakini hata kutolewa kwenye ASFC hivyo kuna kitu wamejifunza kwahiyo itakuwa ngumu kwetu."

"Aucho niwahakikishie yupo fiti kwa ajili ya mchezo wetu wa kesho (leo) dhidi ya Namungo na atakuwepo. Denis Nkane na Aboutwalib Mshery wako katika matibabu ya muda mrefu lakini wengine leo kwenye mazoezi ya mwisho tutaangalia wale ambao tutakuwa nao watatusaidia kesho (leo)," alisema Kaze.

Yanga wanaingia katika mechi ya leo wakiwa na muendelezo wa kufanya vizuri kwenye Ligi ambapo katika mechi 10 zilizopita, wameshinda tisa na kupoteza moja tu huku wakifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne tu.

Hali ni tofauti kwa Namungo ambao wamekuwa na mwenendo wa kusuasua na kuthibitisha hilo, katika mechi zao 10 zilizopita za Ligi, wamepata ushindi mara nne, kutoka sare mbili na kupoteza mechi nne.

Kocha msaidizi wa Namungo, Shadrack Nsajigwa amekiri wanafahamu ubora wa Yanga na wamejipanga kukabiliana na ubora wao.

"Tumewasili jana (juzi) hapa Dar es Salaam. Tuko tayari kwa ajili ya kushindana na wenzetu wa Yanga kuendeleza mapambano yetu ya ligi. Kimsingi mechi itakuwa ngumu. Tunajiamini kama tutacheza vizuri lakini tutawaheshimu Yanga kama timu inayoongoza ligi. Tunajua jinsi ya kuzuia, kushambulia na tunaamini tunaweza kupata kitu katika mchezo wa kesho (leo)," alisema Nsajigwa.

Mchezo mwingine leo utakuwa ni baina ya Dodoma Jiji dhidi ya Azam FC katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma kuanzia saa 2:30 usiku.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live