Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Saleh Ally Jembe amesema kuwa muda waliopewa waliokuwa washambuliaji wa Simba SC, Moses Phiri na Jean Baleke uliwatosha kuonyesha kitu lakini wawili hao walishindwa kabisa kuonyesha chochote.
Jembe amesema hayo baada ya Phiri na Baleke kufungashiwa virago na Simba wakati wa dirisha dogo la usajili hivi karibuni.
“Phiri na Baleke hawakupaswa kupewa nafasi nyingine mbili au tatu, sababu tayari walishapewa nafasi ya kutosha lakini hawakuonyesha kitu. Nilizungumzia ile cheka cheka ya Phiri mkakasirika, nikazungumza kwamba Baleke ana mambo ya kitoto mkakasirika.
“Nadhani hawa walioletwa wapewe video za Baleke na Phiri kuwaoneshakwamba hawa waliokuwa wachezaji wazuri walifeli kabisa na kushindwa kuonyesha chochote ambacho kingewafanya waonekane wanastahili kuvaa jezi ya Simba au kuiwakilisha Simba.
“Wazalendo wengi wangeweza kufanya makubwa zaidi ya walichofanya Phiri na Baleke, kwa hiyo kuondoka kwao ni sawasawa tu. Ulitaka wapewe nafasi ipi? Badala ya kuwa wachezaji wa timu wanataka kuwa kama wamiliki wa klabu.
“Simba walichofanya ni maamuzi magumu na ndiyo hayo waliyokuwa wanayataka wanachama. Maamuzi yao yataonekana mabaya iwapo wachezaji waliowaleta watashindwa ku-perform, watu watakumbushia mambo ya Baleke na Phiri lakini kama hawa wachezaji watafanya vizuri, mashabiki watasahau na kusonga mbele.
“Simba wawe wavumilivu, tunaamini kama wamewaangalia vya kutosha basi itafika wakati watawasaidia. Phiri na Baleke walipewa nafasi ya kutosha lakini wameshindwa, acha waende wakatafute changamoto sehemu nyingine. Huenda Baleke akaenda TP Mazembe akafanya vizuri, Phiri akaenda kwao Zambia akafanya vizuri,” amesema Jembe.