Wakati Simba ikifufuka na kupata ushindi wa kwanza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Wydad Casablanca kwa ushindi wa mabao 2-0, jina la mshambuliaji Moses Phiri liliondolewa wakiwa vyumbani.
Uamuzi wa kukata jina la mshambuliaji huyo ulikuja baada ya kuonekana idadi imezidi na walikuwa wachezaji 22 badala ya 20, idadi iliyotakiwa na hivyo yeye pamoja na Jimyson Mwanuke waliondolewa na kupisha mastaa 20 walioibeba timu hiyo.
Katika hali ya kushangaza kabla ya mchezo kuanza Simba ilishuka na mastaa wao 22, lakini kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika ndani ya Simba kililiambia Mwanaspoti uamuzi uliofanyika chini ya kocha Abdelhak Benchikha ulikuwa ni kuwapunguza wachezaji hao ili kuwa na idadi ya wachezaji 20.
Wachezaji waliokuwa wamebaki ni Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Che Malone, Henock Inonga, Fabrice Ngoma, Kibu Denis, Mzamiru Yassin, Jean Baleke, Clatous Chama na Willy Onana ambao walianza kikosi cha kwanza.
Wengine ni Ally Salim, David Kameta ‘Duchu’, Israel Mwenda, Keneddy Juma, Abdallah Hamis, Hussain Kazi, Luis Miquissone, John Bocco na Shaban Chilunda.
Katika mchezo huo, Simba iliyokuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, iliibuka na ushindi huo wa mabao mawili ya Willy Onana dakika ya 35 na 37, yaliyoipa pointi tatu na kupanda hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi tano kabla ya mchezo wa Asec Mimosas dhidi ya Janeng Gallaxy walio katika kundi moja.