Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Phiri ateka shoo...Mgunda abadili ratiba

Phiri, Chama Straika wa Simba Moses Phiri

Tue, 8 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba tangu majuzi kinafanya mazoezini asubuhi baada ya Kocha, Juma Mgunda kuwabadilishia ratiba mastaa wake, huku Moses Phiri, Clatous Chama na Augustine Okrah waking’ara zaidi ya wenzao, ghafla juzi kocha huyo amewabadilishia tena na kuwarejesha wote kambini.

Mgunda amesema kuwa ameamua kubadilisha tena ratiba baada ya kubaini mechi yao ijayo dhidi ya Singida Big Stars itapigwa jioni hivyo kufanya mazoezi asubuhi ilikuwa ni kama kujivuruga na jana akawaita nyota wote kambini baada ya tizi la mwisho kabla ya leo kusafiri kwenda Singida.

Awali Mgunda alibadili ratiba ya mazoezi aliyokuwa akiwapatia wachezaji wake mara baada ya kutoka kucheza na Mtibwa Sugar kwa kupewa mapumziko kisha kuwapigisha kila siku kuanzia saa 3:00 hadi saa 4:30 asubuhi na kila yalipoisha waliruhusiwa kwenda makwao wakitakiwa kupumzisha miili tu.

Katika mazoezi yaliyokuwa yakifanyika asubuhi na Mwanaspoti kuyashuhudia, Chama, Phiri na Okrah walifunika zaidi kwa wageni, huku Kennedy Juma, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni waking’ara kwa wazawa sambamba na nahodha John Bocco na Mzamiru Yasin.

Katika mazoezi ya Simba yaliyofanyika wiki hii beki wa kulia, Shomary Kapombe ameonekana kurudi kwenye kiwango bora, akitimiza majukumu yake vizuri uwanjani kama alivyokuwa akielekezwa.

Kapombe aliyekuwa majeruhi na kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili alirejea kwenye mchezo wa Mtibwa, ingawa hakucheza kwenye kiwango cha juu, lakini kwenye mazoezi ya timu hiyo alifanya kazi nzuri ya kuwazuia mawinga, Pape Sakho, Okrah na Pater Banda aliokuwa anakabana nao kwenye nyakati tofauti.

Kama hiyo haitoshi Kapombe alikuwa bora kwenye kuanzisha mashambulizi kutokea pembeni alikuwa anapiga krosi na pasi za maana kwa washambuliaji, Moses Phiri, John Bocco na Habibu Kyombo waliokuwa wanazitumia kufunga mabao.

Nyota mwingine aliyekuwa kwenye ubora mazoezini ni Chama kwani tizi la mbinu za kucheza kwa kushambulia mipango yote ilikuwa inaanzia kwake.

Chama alikuwa mtulivu nyakati zote pindi mpira ilipokuwa mguuni kwake alitengeneza shambulizi zuri lililokwenda kuleta hatari au kuzaa bao kama ambavyo Mgunda alivyokuwa anahitaji.

Kiungo huyo fundi nyakati mwingine mbali ya kutengeneza shambulizi kutokana na uwezo wa kufanya hivyo aliokuwa nao pamoja na kupiga pasi alikuwa anafunga.

Alipotafutwa Chama alisema anafanya hivyo kwa ajili ya timu kufanya vizuri mchezo wa mbele yao dhidi ya Singida ili kupata pointi zote tatu kama malengo yao yalivyo.

“Nashukuru Mungu nipo vizuri na naendelea na mazoezi kama vile ambavyo benchi la ufundi linatuelekeza ili kwenda kupata pointi tatu ugenini,” alisema Chama.

Kutokana na ubora wa wachezaji hao wawili kwenye kutengeneza nafasi za kufunga katik mazoezi hayo ya Simba, Phiri naye amekuwa katika moto wa kuendeleza kasi yake ya kufunga.

Kama Kapombe, Chama na Phiri watakuwa na ubora kama walionyesha kwenye mazoezi yao katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars watakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia.

Kwani kila tizi lililokuwa likitolewa na makocha wa timu hiyo yaani Mgunda na wasaidizi wake akiwamo Seleman Matola, nyota hao walionekana kwenda sambamba na kufanya kila mara kupigiwa makofi, hata hivyo wachezaji watatu akiwamo beki Israel Mwenda, winga Jimmyson Mwanuke na kiungo mshambuliaji Nelson Okwa walikosekana kutokana na kuwa majeruhi.

Wachezaji hao, huenda wakaachwa kwenye msafara wa timu hiyo unaoondoka leo kwenda Dodoma kwa ndege kabla ya kunganisha usafiri wa basi hadi Singida itakapopigwa mechi yao ya kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji, Singida Big Stars itakayopigwa keshokutwa Jumatano katika Uwanja wa Liti.

Katika kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye mchezo huo na kupata pointi tatu wachezaji, benchi la ufundi lililo chini ya Mgunda limepanga kuondoka leo jioni, huku basi la kuwabeba wachezaji lilitarajiwa kuondoka jana kutangulia Dodoma ili kuupokea msafara huo wa kwenda Singida.

Chanzo: Mwanaspoti