Mshambuliaji wa Simba, Mzambia, Moses Phiri, amesema kuwa kasi ya mabao aliyoanza nayo kiungo mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ itamfanya arejee kivingine uwanjani.
Phiri mwenye mabao 10, yupo nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha aliyoyapata katika mguu wake wa kulia wakati timu hiyo, ilipovaana na Kagera Sugar.
Saido tangu ajiunge na Simba, amecheza michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara, akipiga asisti mbili, huku akifunga mabao matano ambayo yamemfanya afikishe 9 sawa na John Bocco, huku Phiri akiwa na 10.
Akizungumza nasi, Phiri alisema amefurahishwa na ushindani huo wa washambuliaji wenzake Saido na Bocco ambao utamfanya arejee kwa kasi kubwa baada ya kuruhusiwa kucheza.
Phiri alisema kuwa pongezi nyingi ziende kwa Saido na Bocco ambao wamemuwakilisha vema katika kipindi yeye yupo nje akiuguza majeraha.
“Kiukweli kasi imekuwa kubwa, mshindani wangu katika ufungaji (Fiston Mayele) ameniacha mbali kutokana na mimi kukosa mechi nyingi kutokana na kukaa nje ya uwanja kwa muda.
“Lakini nashukuru kumuona Saido na Bocco wanafanya vizuri, wamekuwa bora wanapofika katika goli la wapinzani na kufunga mabao, kiukweli hii inanipa furaha.
“Kikubwa waendelee kupambana zaidi, kwani kila mmoja amebakiza bao moja ili anifikie, kwangu sio mbaya kwani nacheza nao timu moja,” alisema Phiri.