Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Phiri aliamsha Simba Kwa Mkapa

Phirii Goal.jpeg Phiri aliamsha Simba Kwa Mkapa

Sat, 2 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba kinajiandaa kushuka Uwanja wa Benjamin Mkapa usiku wa leo kuikabili Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya kufungia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku nyota wa zamani wa timu hiyo, Moses Phiri amekiamsha kwa kuwataka wakaze ili timu iendeleze rekodi ya kucheza robo fainali kwa mara nyingine.

Phiri aliyeondoka Simba dirisha dogo akiwa amefunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara, kwa sasa anakipiga kwa mkopo Power Dynamos ya Zambia na licha ya kuwa mbali, bado anaifuatilia chama lake la zamani na anajua leo Saa 1:00 usiku itakapiga na Jwaneng na kuwajaza upepo mastaa wa timu hili wapambane washinde waende robo fainali.

Phiri aliyekuwa sehemu ya kikosi cha Simba msimu uliopita kiilichocheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wydad CA ya Casablanca, amesema anaamini wababe hao wa Tanzania na Afrika Mashariki wanaweza kufuzu.

"Leo ni siku ya wana Simba kufurahi… naitakia timu yangu ya Simba kila la kheri kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Galaxy ili kufika hatua ya robo fainali," ameandika mchezaji huyo kwenye mtandao wake wa kijamii.

Simba yenye pointi sita sawa na Wydad katika Kundi B linaloongozwa na ASEC Mimosas iliyofuzu mapema robo fainali, inahitaji ushindi katika mchezo huo dhidi ya mabingwa wa Botswana ili kutinga hatua hiyo ya robo kwa mara ya nne mfululizo kati ya misimu mitano ya michuano ya kimataifa.

Wafuasi wa mshambuliaji huyo kwenye mtandao wa Instagram wamefurahishwa na chapisho hilo kwa kutoa maoni tofauti kuhusiana na mchezo huo.

Joyce amesema; "Asante General. Wanasimba tunakupenda." Raj Ramson naye ameandika kumuunga mkono Phri kwa kusema,"Tunakupenda sana na naamini utarudi nyumbani na kufanya makubwa, kwetu hakuna majini kama ilivyo upande wa pili, tumemisi sana mabao yako."

Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala' ni miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wameonyesha kupokea kheri ambayo wametakiwa wa Mzambia huyo kwa kujibu 'Nguvu Moja'.

Simba itaikaribisha Jwaneng Kwa Mkapa ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha misimu miwili iliyopita ilipofungwa mabao 3-1 na kung'olewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kutokana na wapinzani wao kunufaika na kanuni ya sheria ya bao la ugenini, kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni sare ya 3-3. Simba ilishinda 2-0 ugenini.

Iwapo Simba itapenya kwenye hatua hiyo, itaifanya Tanzania kwa mara ya kwanza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuingiza timu mbili kwenye hatua hiyo, kwani tayari Yanga ilishatinga kutoka Kundi D na usiku wa jana ilikuwa uwanjani jijini Cairo, Misri kukamilisha ratiba dhidi ya Al Ahly iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0, huku CR Belouizdad ya Algeria iliyopo pia kundi hilo kumaliza makundi kwa kishindo kwa kuifunga Medeama mabao 3-0.

Watetezi Al Ahly imemaliza kama kinara wa kundi ikiwa na pointi 12, ikifuatiwa na Yanga yenye nane kama CR Belouizdad ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, wakati Medeama imemaliza mkiani na alama nne tu.

Chanzo: Mwanaspoti