Dakika 90, za mchezo wa marudiano hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba dhidi ya Nyasa Big Bullets zimetamatika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji kuondoka tena na ushindi mnono wa mabao 2-0.
Mambo yote ya Simba yamewekwa kimiani na kiungo wake mshambuliaji, Moses Phiri dakika ya 29 na 50 ikiwa ni muda mchache tu tangu timu hizo zilipoingia kipindi cha pili cha mchezo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Bullets kufanya mabadiliko ya kuwatoa, McPhallen Ngwira, Anthony Mfune huku nafasi zao zikichukuliwa na Righteous Banda na Adepoju Baba Tunde.
Mabadiliko hayo yaliwachangamsha wageni walioonekana kulishambulia lango la Simba licha ya nyota wake kukosa umakini wa kutumia vizuri nafasi.
Mashambulizi hayo yaliiamsha Simba ambapo dakika ya 50, kiungo mshambuliaji, Moses Phiri aliipatia bao la pili na kuwafanya Bullets chini ya Kocha wao Mkuu Mzimbabwe, Kalisto Pasuwa kushindwa kutegua mtego wa vijana hao wa Mgunda ambao walikuwa katika ubora.
Kufuatia bao hilo Kocha wa Simba, Juma Mgunda alifanya mabadiliko kwa kuwatoa mshambuliaji Kibu Denis ambaye hakuwa na mchezo mzuri na Augustine Okrah huku nafasi zao zikichukuliwa na Pape Ousmane Sakho na Peter Banda.
Simba iliendelea kufanya mabadiliko kwa kuwatoa, Moses Phiri, Sadio Kanoute, Henock Inonga na nafasi zao kuchukuliwa na Nelson Okwa, Mohamed Ouattara na Dejan Georgejivic.
Mabadiliko hayo ya Mgunda yalionekana ya kiufundi zaidi kwa Simba ambayo ilikuwa ikitengeneza balansi nzuri kuanzia eneo la kujilinda hadi like la ushambuliaji lililoongozwa na Dejan baada ya kuingia katika kipindi cha pili.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufuzu hatua ya pili kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba 11, kushinda pia 2-0.
Baada ya ushindi huu sasa Simba itakutana na mshindi wa jumla katika raundi ya pili kati ya Red Arrows ya Zambia dhidi ya Primeiro de Agosto kutoka Angola, mchezo utakaopigwa muda mchache kuanzia sasa huku Primeiro ikiwa na mtaji wa kuongoza bao 1-0, ililolipata wiki iliyopita.
Kikosi kamili cha Simba kilichoanza ni, Aishi Manula, Israel Mwenda, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Kennedy Juma, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Kibu Denis, Mzamiru Yassin, Moses Phiri, Clatous Chama na Augustine Okrah.
Wachezaji wa akiba ni, Beno Kakolanya, Erasto Nyoni, Mohamed Ouattara, Jonas Mkude, Pape Sakho, Nelson Okwa, Dejan Georgijevic, John Bocco na Peter Banda.
Kikosi cha Nyasa Big Bullets kilichoanza ni, Clever Mkungulu, John Lanjesi, Precious Mavuto Sambani, Hassan Kajoke, Charles Petro, Alick Lungu, Gomezgan Chirwa, Henry Kabichi, Patrick Phiri, Anthony Mfune na MacFarlen Mgwira.
Wachezaji wa akiba ni, Nickson Nyasulu, Blessings Mpokera, Chimwemwe Idana, Righteous Banda, Adepoju Babatunde, Richard Chimbamba, Kesten Simbi, Patrick Mwaungulu na Frank Willard.