Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Phiri aipa pigo Simba, Mwenda aisubiri Dar

Local Simba.jpeg Phiri aipa pigo Simba, Mwenda aisubiri Dar

Sat, 24 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati beki Israel Mwenda akipona majeraha yake, safu ya ushambualiaji ya Simba imepata doa baada ya nyota wake Moses Phiri kupata majeraha yatakayomuweka nje katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, keshokutwa utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Phiri anayeongoza kwa kufumania nyavu katika kikosi cha Simba kwenye ligi alipata majeraha hayo katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, juzi.

Kutokana na majeraha hayo kuna wasiwasi pia wa nyota huyo kukosa mchezo utakafuata baada ya hapo dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, Desemba 30.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliliambia gazeti hili kuwa katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Phiri alipata majeraha ambayo yamemfanya nyota huyo kutomudu hata kutembea vizuri.

“Kwenye mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar, mshambuliaji Moses Phiri alifanyiwa faulo ambazo zilisababisha apate majeraha na hapa ninapozungumza na wewe tumerejea Mwanza, lakini hata kukanyaga chini hawezi jambo lililomfanya atembee kwa usaidizi wa magongo,” alisema Ally.

“Baada ya kuwasili Mwanza tumeshampeleka hospitali kwa ajili ya vipimo ambavyo leo (jana) jioni vitatoka ili kubaini ukubwa wa tatizo lake na kufahamu muda ambao atakaa nje, hivyo tutamkosa katika mechi yetu dhidi ya KMC. Hata hivyo wachezaji wengine wote ambao wameambatana na timu Mwanza ukiondoa Phiri wako vizuri na leo (jana) tutaanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu unaofuata.”

Phiri amekuwa tegemeo la Simba katika safu ya ushambuliaji kutokana na uwezo mkubwa ambao amekuwa akiuonyesha katika kufumania nyavu ambapo kwenye Ligi Kuu ameshaifungia mabao 10 yanayomfanya ashike nafasi ya pili katika orodha ya wafumania nyavu kwenye ligi nyuma ya Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 13.

Katika Kombe la Shirikisho la Azam, Phiri pia anashika nafasi ya pili katika chati ya ufungaji bora akiwa amepachika mabao manne huku kinara akiwa ni Andrew Simchimba mwenye mabao matano. Kuumia kwa Phiri hapana shaka kunaiongezea Simba presha ya kusajili mshambuliaji mpya kipindi hiki cha uhamisho kwani kwa sasa imebaki na washambuliaji wawili wa kati ambao ni John Bocco na Habibu Kiyombo.

Akizungumzia majeraha ya Phiri, kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema kuwa wamejipanga kukabiliana na KMC pasipo uwepo wa nyota huyo.

“Tunawaachia timu ya madaktari ili apate matibabu sahihi. Wachezaji wapo na wenye uwezo hivyo uwezekano wa kuziba nafasi hiyo na watu wa kucheza wapo,” alisema Mgunda.

Hata hivyo, Ally aliwatangazia habari njema Simba ya urejeo wa beki Israel Mwenda ambaye alikaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti.

“Israel ameshapona majeraha yake na sasa ameshaanza mazoezi mepesi, lakini tulimuacha Dar es Salaam hivyo ataungana rasmi na timu ikisharejea baada ya mechi dhidi ya KMC. Majeruhi mwingine ambaye hakusafiri na timu ni Peter Banda ambaye kwa mujibu wa ripoti ya daktari, atakuwa fiti ifikapo Januari,” alisema.

Chanzo: Mwanaspoti