Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Phiri: Chama? Pigeni chini

Phiri: Chama Phiri: Chama? Pigeni chini

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati kiungo Clatous Chama akisubiri kufikishwa Kamati ya Nidhamu baada ya kusimamishwa na uongozi kwa madai ya utovu wa nidhamu, kocha wa zamani wa timu hiyo, Patrick Phiri amesema mabosi wa klabu hiyo wanapaswa kuchukua hatua zaidi ili kulinda heshima ya klabu yao ikiwemo kuamua kuachana naye kabisa.

Simba ilitangaza kumsimamisha Chama na Nassor Kapama kwa utovu wa nidhamu, ikielezwa watapelekwa kwenye kamati hiyo ya nidhamu iliyopo chini ya Kamanda Mstaafu wa Polisi, Seleman Kova.

Hata hivyo, Phiri aliyewahi kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara misimu miwili tofauti ukiwamo ule wa bila kupoteza 2009-2010 aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Zambia, inasikitisha kuona mchezaji mkubwa kama Chama kupata tuhuma hizo, huku akisisitiza endapo itabainika ni kweli basi mabosi wa Simba wanapaswa kufanya maamuzi magumu juu ya nyota huyo.

Phiri ambaye pia ni raia wa Zambia alisema, Chama ni mchezaji mzuri, lakini sasa zama zake zimeanza kuisha kilichobaki ni uzoefu tu unaombeba, hivyo kupata tuhuma hizo nako kunamshusha zaidi ubora wake.

“Inasikitisha kusikia Chama anasimamishwa kwa utovu wa nidhamu, nidhamu ni msingi wa mafanikio ndani ya Simba na popote pale. Simba ni timu kubwa ina uzoefu wa kuiendesha timu, pia ina watu sahihi wa kusahihisha ukosefu wa nidhamu na kuongeza hamasa katika timu na kuwatia moyo wachezaji na mashabiki. Pengine Chama amekuwa mkubwa zaidi ya klabu kitu ambacho ni kibaya sana ikishindikana kumaliza suala lake la nidhamu basi waachane naye waijenge timu,” alisema Phiri na kuongeza;

“Viongozi wa Simba sasa wakae chini kila mmoja na kujielekeza vyema zaidi na kushinda ligi na vikombe kwa mara nyingine. Hivi ndivyo tunavyoijua Simba. Simba itabaki kuwa Simba siku zote. Timu ambayo inashinda na kushinda na kushinda lakini asiwepo mchezaji wa kuwa juu ya taasisi ama klabu, hii itasaidia kuleta mafanikio ndani ya timu.

“Kipindi hiki Simba itakuwa inapitia kipindi kigumu, jambo ambalo ni kawaida katika klabu, ila nina imani itafufuka tena, ina uwezo wa kushinda kwani kila unapoanguka kumbuka unainuka tena na kupigana kwa nguvu zaidi ndio maana inaitwa Simba, hivyo kwa mchezaji ambaye ana utovu wa nidhamu iangalie namna ya kudili naye na ikiwezekana iachàne naye ili kujenga misingi mizuri ya klabu.”

Chama anatuhumiwa kumtolea lugha chafu kocha wa viungo wakati timu hiyo ilipofanya mazoezi ya kupasha miili ikijiandaa kucheza na Wydad mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

“Hata kama mchezaji unaona unakwazwa na jambo fulani basi mtafute mshauri mwenye busara wa kuzungumza naye kabla hujafanya maamuzi, inawezekana kuna tofauti binafsi lakini huwezi kuleta tofauti zako mahali pako pa kazi. Watu wanapokuwa Simba lazima kila mtu atangulize Simba na kuzika sintofahamu binafsi,” alisema Phiri.

Kwa upande wa Kapama anadaiwa kutokwenda mazoezini huku ikielezwa anataka atolewe kwa mkopo kwani amechoka kufanya mazoezi pasipo kucheza mechi za mashindano. Tangu msimu huu uanze Kapama hajacheza mechi hata moja.

Simba imecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara huku kimataifa ikicheza mechi nne ikishika nafsi ya pili Kundi B ikisaliwa na michezo miwili dhidi ya Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy, itakayopigwa kati ya Februari 23 na Machi 2 mwakani.

Chanzo: Mwanaspoti