Kiwango kisichoridhisha cha Moses Phiri na Jean Baleke kwenye Kombe la Mapinduzi hasa katika mechi ya fainali dhidi ya Mlandege juzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kimemkwaza kocha Abdelhak Benchikha ambaye amekiri hadharani kuwa anahitaji walio bora kuliko wawili hao.
Katika mechi sita za Kombe la Mapinduzi ambazo Simba imecheza, Baleke na Phiri kila mmoja amefunga bao moja huku Simba ikimaliza ikiwa imefunga mabao saba.
Wachezaji hao wawili ambao wamekuwa wakitumika katika nafasi ya mshambuliaji wa kati, walionyesha ubutu wa kutumia nafasi kwa kupoteza nafasi nyingi ambazo timu hiyo ilikuwa ikitengeneza.
Benchikha alisema kuwa mchezo wa mwisho dhidi ya Mlandege umedhihirisha wazi kuwa washambuliaji wake wameshindwa kufanya kile ambacho anakitarajia kutoka kwao ambacho ni kufunga mabao
Mbali na upande wa ushambuliaji, Benchikha alisema hata nafasi ya kiungo cha ushambuliaji nayo imeonyesha changamoto hivyo nayo inapaswa kuwa kipaumbele katika mipango ya usajili ya timu hiyo.
“Tumekosa washambuliaji wenye nguvu na ubora na hii ni Simba ni timu kubwa. Inahitaji mshambuliaji imara kwa vile inashiriki mashindano makubwa.
“Washambuliaji hawakuwa vizuri na pia hatuna kiungo wa ushambuliaji anayeweza kutengeneza nafasi za mabao. Ukiangalia mchezo dhidi ya Mlandege baada ya wapinzani kupata bao walirudi nyuma kulinda na tukashindwa kuwafungua,” alisema Benchikha.
Kocha huyo amesisitiza kuwa timu yake inapaswa kufanya usajili imara wa nafasi ambazo zimeonyesha udhaifu kama inahitaji kufanya vyema katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
Akizungumzia kauli hiyo ya kocha Benchikha, mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema kuwa uongozi utafanyia kazi kila ambacho Benchikha na benchi lake la ufundi litapendekeza.
“Uongozi jukumu letu ni kutimiza kile ambacho timu inakihitaji na kama ambavyo tuliahidi kwamba kila ambacho benchi la ufundi linakihitaji tutahakikishia tunalipatia. Usajili kocha ndo mwamuzi.”