Philippe Coutinho sasa anaripotiwa kuwa tayari kujiunga na Newcastle United mwaka ujao, baada ya kukubali kwamba hana muda mrefu Barcelona.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 aliona nyavu kwenye ushindi wa 3-1 wa timu yake dhidi ya Villarreal kwenye mechi ya ligi Jumamosi na amecheza mechi 13 katika mashindano yote akiwa na wababe hao msimu huu.
Coutinho anaripotiwa kutokuwepo kwenye mipango ya Xavi pale Barcelona, hata hivyo, na mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil anatarajiwa kuondoka Camp Nou mwezi Januari au wakati wa usajili wa majira ya joto.
Newcastle wamekuwa wakihusishwa na mchezaji huyo tangu kukamilika kwa utawala wao wa Saudia, lakini awali ilifikiriwa kuwa Coutinho hakuwa tayari kufikiria kuhamia Newcastle.
Kwa mujibu wa El Nacional, Coutinho sasa amebadili mawazo yake juu ya kuhamia timu ya Eddie Howe na yuko tayari kujadili uhamisho wake kwenda St James’ Park.
Ripoti hiyo inadai kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool anataka kurejea Ligi Kuu ya Uingereza na anajua kwamba angepokea mshahara mkubwa kwa kuhamia Newcastle.
Coutinho kwa kiasi kikubwa amekuwa na wakati mgumu kuonesha kiwango bora Barcelona tangu alipowasili kutoka Liverpool Januari 2018.