Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Petr Cech aliwabeba kina John Terry

GettyImages460331504 3308074 Petr Cech aliwabeba kina John Terry

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kipa raia wa Jamhuri ya Czech, Petr Cech, alisajiliwa na Chelsea mwaka 2004 na alidumu na klabu hiyo kwa miaka 11, hadi alipoondoka mwaka 2015.

Katika kipindi hicho, Cech alikabiliana na mashuti 1241 yaliyolenga lango. Aliokoa mashuti 1000 huku akiyashindwa mashuti 241 pekee ambayo yalitinga kimiani.

Takwimu hizo ni pamoja na msimu wake wa kwanza wa 2004/05 ambao aliruhusu mabao 15 tu kwenye mechi 35 za ligi kuu.

Msimu huo Chelsea walipoteza mchezo mmoja tu lakini hata hivyo, walishinda mechi 11 kwa ushindi finyu wa 1-0 ambao kwa asilimia nyingi ulipatikana kutokana mikono salama ya Petr Cech.

Kwa sababu ili matokeo yabaki 1-0 hadi mwisho, ilitakiwa Cech aokoe michomo kadhaa ya hatari. Rekodi hizi zinamfanya Cech aonekane alikuwa kipa bora sana na anastahili kuonekana hivyo.

Mtandao maarufu wa michezo wa Sportsbible unamtaja Petr Cech kama kipa namba sita katika orodha ya makipa bora wa muda wote.

KUMI BORA

1. Levy Yashin - Urusi

Huyu anatajwa kuwa kipa bora wa muda wote duniani. Katika maisha yake ya soka, aliokoa penati 150. Ndiyo kipa pekee kuwahi kushinda Balon d’Or.

Tuzo ya kipa bora ya Balon d’Or inaitwa Levy Yashin kwa heshima ya mwamba huyu.

2. Iker Casillas - Hispania

3. Gianluigi Buffon - Italia

4. Dino Zoff - Italia

5. Manuel Neuer - Ujerumani

6. Petr Cech - Jamhuri ya Czech

7. Oliver Khan - Ujerumani

8. Peter Schmeichel

9. Edwin van der Sar - Uholanzi

10. Gordon Banks - England

Katika orodha hiyo pia, Petr Cech anatajwa kuwa kipa bora wa muda wote wa Ligi Kuu England.

Petr Cech ndiye kipa pekee katika historia ya ligi kuu ya England kupata hati zaidi kuanzia 10 katika msimu mmoja kwa misimu 10.

Cech na Chelsea

2004/05

Mechi 35

Hati safi 24

2005/06

Mechi 34

Hati safi 17

2006/07

Mechi 20

Hati safi 13

2007/08

Mechi 26

Hati safi 14

2008/09

Mechi 35

Hati safi 19

2009/10

Mechi 34

Hati safi 16

2010/11

Mechi 38

Hati safi 14

2011/12

Mechi 34

Hati safi 10

2012/13

Mechi 36

Hati safi 13

2013/14

Mechi 36

Hati safi 14

2014/15

Mechi 7

HATI SAFI 5

Cech anayetajwa hapa na marekodi yake yote haya, alikuwa akilindwa na mabeki bora kama John Terry, Ricardo Carvalho, William Galas, Ashley Cole, Cesar Azipiliqueta, Branislav Ivanovic na kadhalika.

Katika safu ya kiungo cha ulinzi kulikuwa na wababe kama Cloude Makelele, Michael Essien, John Mikel Obi, na kadhalika. Wanaume hawa wanatajwa kama moja ya miamba imara zaidi ya ulinzi katika kizazi chao.

Unaweza ukahitimisha kwa kusema kwamba alifaidika na ukuta wake.

LAKINI...

Inawezakana vipi miamba hawa wa ulinzi walishindwa kumlinda kipa wao kiasi cha kukutana na mashuti yote hayo?

Hapo ndipo panapokuja hoja ya kwamba hawa jamaa siyo kwamba walikuwa bora kama wanavyosifiwa bali walifichiwa sana makosa yao na Cech.

Yaani Cech alitembea kilomita nyingi kuficha udhaifu wao. Kwa mfano mwaka 2012 Chelsea ilishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa penati dhidi ya Bayern Munich.

Katika mchezo huo ukiacha michomo ya kawaida ndani ya mchezo, Cech aliokoa penati tatu; moja ndani ya muda wa mchezo katika dakika 30 za ziada iliyopigwa na Arjen Robben, na mbili katika ile mikwaju ya uamuzi kutoka kwa Ivica Olic na Bastian Schweinsteiger.

Zaidi ya hapo, Cech alizifuata penalti zingine zote, japo ziliingia.

Lakini ili kuokoa penalti hizo ilimbidi awekeze akili na muda wake mwingi kwani alitumia saa nane kuisoma Bayern Munich inavyopiga penalti.

Alichukua penalti za Bayern Munich za miaka mitano nyuma, akaiangalia penalti moja hadi nyingine, hadi zote zikaisha.

Itakumbukwa Bayern Munich walifika fainali hiyo kwa kuitoa Real Madrid kwa penalti tena katika uwanja wa ugenini. Kwa hiyo penalti dhidi ya Chelsea katika fainali iliyofanyika katika uwanja wa nyumbani wa Bayern Munich, zilionekana zingekuwa nyepesi kwao, lakini Cech alikuwa na mipango yake.

Huyu ndiye Petr Cech aliyefanya kila kilichotakiwa kufanywa ili nyavu zake ziwe salama. Ukitaka kuona kwamba mabeki wa Chelsea hawakustahili sifa walizopewa wakati ule waangalie walipocheza bila Cech hasa wakiwa na timu zao za taifa. Kituko.

Sisemi kwamba hawakuwa mabeki wazuri, la hasha, lakini sifa nyingi walizopata zilitokana na uimara wa kipa huyo. Cech alicheza mechi 494 akiwa Chelsea na kukutana na hayo mashuti 1241 kwa miaka 11. Hii ina maana kwamba wapinzani walimfikia mara nyingi zaidi, lakini alisimama imara.

Endapo kina John Terry wangecheza na makipa legelege tungekuwa tunazungumza tofauti tunapowakumbuka kina Ricardo Carvalho.

Chanzo: Mwanaspoti